Michezo

Barcelona wamtwaa beki Sergino Dest kutoka Ajax

October 1st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BEKI wa kulia Sergino Dest ameingia katika sajili rasmi ya Barcelona baada ya kuagana rasmi na kikosi cha Ajax cha Ligi Kuu ya Uholanzi kwa kima cha Sh2.5 bilioni.

Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 19 alipokezwa malezi ya soka katika akademia ya Ajax na akaanza kuwajibishwa katika kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Uholanzi mnamo 2019.

Dest alizaliwa nchini Uholanzi na amewahi kuchezea timu ya taifa ya Amerika katika kiwango cha chipukizi.

“Sergino amefanyiwa vipimo vya afya uwanjani Camp Nou na ametia saini mkataba wa muda mrefu,” akasema kocha mpya wa Barcelona, Ronald Koeman aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Quique Setien aliyetimuliwa mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20.

Kufikia sasa, Barcelona wameagana na wanasoka Arthur Melo aliyetua Juventus, Ivan Rakitic aliyejiunga na Sevilla na Nelson Semedo aliyeyoyomea Wolves.

Wengine ni Arturo Vidal aliyesajiliwa na Inter Milan na Luis Suarez aliyeingia katika sajili rasmi ya Atletico Madrid. Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, ni wachezaji Marc-Andre ter Stegen, Gerard Pique, Frenkie de Jong, Antoine Griezmann, Lionel Messi na chipukizi Ansu Fati pekee ambao wana uhakika wa kusalia kambini mwa Barcelona.

Wachezaji wengine ambao wanatarajiwa kuagana rasmi na Barcelona muhula huu ni Jean-Clair Todibo, Rafinha, Junior Firpo, Todibo, Samuel Umtiti na Ousmane Dembele.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO