Michezo

Barcelona wamwajiri kocha Koeman kuwa mrithi wa Setien

August 19th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

RONALD Koeman amepokezwa mikoba ya Barcelona siku mbili baada ya miamba hao wa soka ya Uhispania kumtimua mkufunzi Quique Setien.

Koeman, 57, amesajiliwa na Barcelona kwa miaka miwili baada ya kushawishiwa kuagana na timu ya taifa ya Uholanzi wakati akisalia na miaka miwili kwenye mkataba wake na kikosi hicho.

Koeman aliwahi kuchezea Barcelona kati ya 1989 na 1995 na akawasaidia kunyanyua mataji manne ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na moja la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Katika kampeni za msimu huu, Barcelona walikamilisha kampeni za La Liga katika nafasi ya pili na kukosa kutwaa taji kwa mara ya kwanza tangu 2007-08.

Pengo la alama tano lililodumu kati ya Barcelona na Real Madrid na kichapo kikali cha 8-2 ambacho kikosi hicho kilipokezwa na Bayern Munich kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu, ni kiini cha Barcelona kukatiza uhusiano wao na Setien.

Barcelona pia walimtangaza Ramon Planes kuwa mkurugenzi mpya wa kiufundi kambini mwao. Planes alikuwa msaidizi wa Eric Abidal aliyetimuliwa na Barcelona akiwa mkurugenzi wa spoti.

Koeman alianza safari yake ya ukufunzi akiwa msaidizi wa Guus Hiddink katika timu ya taiga ya Uholanzi na kwa pamoja, wakakiongoza kikosi hicho kwenye fainali za Kombe la Dunia mnamo 1998. Baada ya hapo aliaminiwa kuwa kocha msaidizi wa Louis van Gaal kambini mwa Barcelona kati ya 1998 na 2000.

Alirejea baadaye nchini Uholanzi alikodhibiti mikoba ya klabu za Ajax na PSV. Akiwa kocha wa Valencia alikohudumu kwa kipindi kifupi mnamo 2007, Koeman aliongoza kikosi hicho kutwaa ubingwa wa Copa del Rey. Alitimuliwa baada ya kikosi hicho kukamilisha msimu huo wa La Liga katika nafasi ya 17 kwa alama mbili pekee nje ya mduara wa klabu zilizoshuka daraja.

Baada ya kuhudumu pia kambini mwa AZ Alkmaar na Feyenoord, Koeman alipokezwa mikoba ya Southampton mnamo 2014 alikowasaidia kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza katika nafasi ya sita na saba zilizowakatia tiketi ya kushiriki kivumbi cha Europa League.

Everton walimsajili mnamo 2017 ila akahuhumu uwanjani Goodison Park kwa miezi 16 pekee kabla ya kufutwa na kikosi hicho kilichoambulia nafasi ya 17.

Licha ya matokeo duni yaliyosajiliwa na Everton chini ya ukufunzi wa Koeman, kocha huyo aliajiriwa na timu ya taifa ya Uholanzi mnamo Februari 2018. Uholanzi walihitaji ufufuo mkubwa baada ya kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi.

Chini ya Koeman, Uholanzi walitinga fainali ya Uefa Nations League mnamo 2019 na akawasaidia kufuzu kwa fainali za Euro 2020.

13 Januari 2020 Quique Setien anaajiriwa na Barcelona kwa mkataba wa miaka miwili na nusu kuwa mrithi wa mtangulizi wake Ernesto Valverde.
19 Januari 2020 Setien anasajili ushindi katika mechi yake ya kwanza ligini inayoshuhudia Lionel Messi akifunga bao la pekee katika ushindi huo wa 1-0 dhidi ya Granada.
6 Februari 2020 Barcelona wanaondolewa na Athletic Bilbao kwenye Copa del Rey katika hatua ya robo-fainali.
1 Machi 2020 Barcelona wanapoteza El Clasico dhidi ya Real Madrid ambao wanapaa hadi kileleni mwa jedwali la La Liga baada ya kuwaruka Barcelona
16 Julai 2020 Barcelona wanapoteza ubingwa wa La Liga na rekodi ya kutoshindwa kwenye mechi 30 za nyumbani ugani Camp Nou inatamatishwa na Osasuna wanaowapiga 2-1.
14 Agosti 2020 Barcelona wanadhalilishwa na Bayern Munich 8-2 kwenye robo-fainali za UEFA.
17 Agosti 2020 Barcelona wanamfuta kazi kocha Quique Setien.
18 Agosti 2020 Ronald Koeman anafichua azma ya kuwa mrithi wa Setien na Barcelona wanaagana na mkurugenzi wa spoti Eric Abidal.
19 Agosti 2020 Koeman anapokezwa rasmi mikoba ya Barcelona.