Michezo

Barcelona wasema hawamtaki Griezmann

April 16th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MABINGWA watetezi wa Ligi ya Uhispania (La Liga) Barcelona FC, wamepuuzilia mbali taarifa kwamba wanalenga kutwaa huduma za nyota wa Atletico Madrid Antoinne Griezmann mwisho wa msimu huu wa 2018/19.

Hata hivyo, Rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu amesema hawamtaki Griezmann na akatangaza kuwa watarusha ndoano kwa nahodha wa Ajax ya Uholanzi Mattijs de Ligt ambaye umahiri wake kwenye safu ya ulinzi unaendelea kuvutia baadhi ya klabu mahiri Barani Uropa wanaosaka huduma zake.

Griezmann alihusishwa sana na Barcelona kabla ya kipute cha Kombe la Dunia mwaka wa 2018 lakini akasema wazi anaheshimu mkataba unaomweka ugani Wanda Metropolitano hadi 2023.

“Griezmann ni mchezaji wa Atletico Madrid na ana kandarasi nao . Nafurahi kwamba wachezaji mahiri wanapatikana Uhispania, hali inayoongezea Laliga umaarufu na udhamini. Iwapo Griezman angependa kujiunaga nasi basi lazima azungumze na makocha wa timu zote mbili. Hata hivyo jina lake haliko kwenye orodha ya wachezaji tunaolenga kuwasajili,” akasema Bartomeu.

”Mchezaji ambaye tunalala na kuamka tikimfikiria ni De Ligt ambaye mtindo wake wa usakataji gozi unaoana na wetu. Hata hivyo hatujaanzisha mazungumzo na Ajax kumhusu japo tuna nia kubwa ya kutaka huduma zake ugani Camp Nou,” akaongeza Bartomeu.

Barcelona tayari wamekubali kumsajili Frenkie de Jong ambaye pia anawajibikia Ajax. “Tulitaka kumsajili De Jong wakati wa dirisha dogo la uhamisho lakini tulikumbana na ushindani mkali kutoka kwa timu nyinginezo. Tunashukuru tulihimili hilo na hatimaye kumtwaa,” akafichua Bartomeu.

Barcelona wapo pazuri kutwaa ubingwa wa La Liga Santander msimu wa 2018/19 na pia wana nafasi kubwa ya kufuzu nusu fainali ya Klabu Bingwa Barani Uropa baada ya kuchapa Manchester United 1-0 ugani Old Trafford.