Habari Mseto

Barclays yazindua apu kuwapa wateja mikopo

March 20th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Benki ya Barclays imezindua matumizi ya teknolojia ya simu ambayo yatasaidia wawekezaji wadogo kupata mikopo kwa njia ya simu.

Hii ni katika mpango wa benki hiyo kuimarisha viwango vyake vya mikopo. Benki hiyo ilichukua hatua hiyo kuambatana na mabadiliko yanashuhudiwa katika sekta ya benki na mwamko wa matumizi ya teknolojia mpya katika sekta hiyo.

Watumiaji wa huduma za benki hivi sasa wanaweza kuweka pesa au kuchukua katika akaunti zao za benki kwa kutumia simu.

Utafiti uliofanywa Februari na McKinsey katika mataifa sita ya Afrika ulionyesha kuwa asilimia 53 ya wateja wa benki hupenda kutumia intaneti au simu kutoa au kuweka pesa benki wakilinganishwa na asilimia 26 ya watu ambao hupenda kwenda benki kutekeleza shughuli hiyo.

Benki hiyo imezindua apu, Timiza, kwa lengo la kuwarahishia wateja wake kazi. Apu hiyo inalenga watumiaji wa simu, wafanyibiashara wadogo na wajasiriamali.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa Barclays Jeremy Awori, benki hiyo inalenga kusalia maarufu katika sekta ya benki na kuimarisha utoaji wa huduma zake wakati huu ambapo biashara imekuwa ya kidijitali.