Makala

Barua kuzima wanafunzi Mlima Kenya kumlaki Rais yazua gumzo

March 7th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

MTINDO wa wanasiasa na wasimamizi wa taasisi kama makanisa na shule kufungia msafara wa Rais aliye mamlakani nchini Kenya ili kuwasilisha malilio yao ya kuhitaji misaada mbalimbali si mgeni.

Lakini hilo kwa sasa katika eneo la Mlima Kenya limeharamishwa, waliolengwa pakubwa wakiwa ni walimu wakuu.

Walimu wameonywa rasmi kwamba watakuwa wakichukuliwa hatua za kinidhamu kila wakati wanafunzi wao watakapofungia msafara wa Rais William Ruto ili kumlilia.

Katika barua kutoka kwa Afisi ya Rais ambayo imetumwa kwa wakurugenzi wa elimu katika eneo hilo kupitia kwa makamishna wa kaunti, walimu hao wakuu wanaonywa kwamba haitakubalika wanafunzi kuwa wakifungia Rais Ruto barabarani wakimpasha malilio yao.

“Mnafahamishwa kuhusu barua ya kutoka kwa Afisi ya Rais kupitia Mshirikishi wa Eneo la Kati Fred Shisia ikiwa ni RC/SEC/SECU/1/VOL.IX/ ya Februari 23, 2024, ambayo iliangazia kero ya wanafunzi kumfungia Rais Ruto barabarani,” barua hiyo ikaanza.

Ilieleza kwamba mnamo Februari 14 na Februari 16, 2024, Rais Ruto alipotembelea eneo hilo, kulizuka visa kadhaa vya wanafunzi kusimama barabarani na kufungia msafara wake huku wengine wakinaswa ndani ya mabasi wakielekea katika mikutano ambayo kiongozi huyo wa taifa alitarajiwa kuhutubia wenyeji.

“Wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Kirenga, wenzao wavulana wa Kirenga na pia wale wa shule ya msingi, walisimama barabarani na kumfungia Rais,” barua hiyo ikasema.

Iliongeza kwamba kisa cha pili kilihusisha Shule ya Upili ya Munyu-ini ambapo wanafunzi wake walipiga foleni katika mkondo wa msafara wa rais wakiwa wamebeba mabango yaliyoashiria nia ya kujitafutia masilahi yao licha ya kuwa walikuwa wameonywa na maafisa dhidi ya kufanya hivyo.

Aidha, barua hiyo inasema kwamba mabasi ya shule za upili za Muhoho, St Rita Wamwangi na Mahiga, yalinaswa na polisi yakiwa yamebeba wanafunzi ambao maafisa walikisia walikuwa na nia ya ukora wakisafirishwa kuhudhuria hafla ya Rais Ruto katika ziara hiyo.

Aidha, barua hiyo ilisema kwamba wanafunzi wakiwa na sare rasmi za shule walisafirishwa hadi mkutano wa Rais Ruto katika eneo la Kinale wakati ambapo ulikuwa ni wa saa za masomo “wakiwa hawana mwaliko wowote wala ruhusa”.

“Hizo tabia zinakiuka utaratibu uliowekwa ambapo walimu wakuu wanakaidi maagizo yaliyotolewa kwa nia ya kuelekeza watoto katika njia za utundu, utapeli na ukiukaji wa sheria,” ikaeleza barua hiyo.

Katika hali hiyo, wakurugenzi wa elimu mashinani Mlima Kenya walielezewa kwamba “nia kuu ya waraka huu ni kuwaambia muwaelezee walimu wenu wakuu wote katika maeneobunge yote husika kwamba watakuwa wakichukuliwa hatua za kinidhamu katika kiwango cha mtu binafsi iwapo wanafunzi wao watanaswa wakifungia msafara wa Rais Ruto”.

Baadhi ya walimu wakuu walioongea na Taifa Leo walidai wanasiasa ndio hushinikiza walimu wakuu wawatoe wanafunzi darasani ili wakamlaki kiongozi wa nchi.

Mmoja wa walimu hao wakuu aliambia Taifa Leo kwamba “kuna wanasiasa ambao ili wapate umaarufu wa kisiasa, hutushinikiza tuwape wanafunzi wetu ili Rais akisimama kuwalaki kuwe na jumbe za kisiasa na pia wapate manufaa ya kiserikali”.

“Mimi binafsi shule yangu ilipata basi na pia Sh1.2 milioni za kujenga maabara kupitia mbinu ya mbunge kutuelekeza tufunge barabara Rais akipita ndipo apewe malilio yetu,” akasema mwalimu huyo.

Alisema kwamba vitengo vya usalama vinaingilia mpangilio wa siasa mashinani ambapo mbinu ya kutumia watoto huuza sera sana na pia kuunda daraja la chaguzi za siku za usoni.

“Wanafunzi hao wakiwa Kidato cha Lwanza katika utawala wa mwaka wa kwanza wa serikali yoyote iliyoko mamlakani, watakutana baada ya miaka mitano wanafunzi hao wakiwa ni wapigakura,” akaongeza.

Seneta wa Murang’a Joe Nyutu ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Elimu aliambia Taifa Leo kwamba “tutasaka mazingara halisi ya wito huo ili tupate ukweli kamili”.

“Tangu jadi wanafunzi hutangamana na marais pasipo hiyo kasumba ya kudhaniwa kuwa na nia ya utapeli na si busara hasa kutumia lugha ambayo nimeona katika barua hiyo kiasi cha kuita watoto walio na sare rasmi ndani ya mabasi rasmi ya shule, ‘wahuni’,” akasema Bw Nyutu.

Bw Nyutu alisema kamati yake itatafuta msimamo rasmi kutoka kwa Wizara ya Elimu na pia wasimamizi wa Ikulu “kwa kuwa vile kitengo hiki cha usalama kimepakia ujumbe, ni kana kwamba kuna mzozo kati ya Ikulu na watoto wa shule”.

Bw Nyutu alisema kwamba ainajua kwa uhakika kwamba Rais Ruto mwenyewe akipata huo ujumbe wa maafisa wake wa nyanjani, atajieleza kinaga ubaga.

“Niko na uhakika atakuwa katika msimamo wa kudumisha uhusiano wake mwema na watoto wa taifa hili pasipo kuwadhania kwamba wako kwa mwelekeo potovu,” akamalizia Bw Nyutu.

[email protected]