Michezo

Baryan apeperusha bendera ya Kenya tena Mbio za Magari Afrika

August 6th, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

DEREVA Manvir Baryan aliendeleza uweledi wa Kenya katika Mbio za Magari za bara Afrika baada ya kutwaa taji la mwaka 2019, wikendi.

Baryan, ambaye aliibuka bingwa wa mashindano haya ya duru ya saba mwaka 2017 na 2018, alihifadhi taji lake baada ya kuandikisha ushindi wake wa tatu msimu huu aliponyakua taji la Pearl Rally nchini Uganda.

Akishirikiana na mwelekezi wake Drew Sturrock kutoka Scotland, Baryan alishinda duru ya Pearl kwa urahisi. Katika gari lao la aina ya Skoda Fabia, walidhibiti duru ya Uganda kutoka mwanzo hadi mwisho.

Baryan alifungua msimu kwa kutwaa taji la Bandama Rally nchini Ivory Coast mwezi Februari.

Alitetea taji lake la Zambia Rally mwezi Juni na kumaliza Safari Rally katika nafasi ya tatu nchini Kenya mwezi Julai, ingawa katika nafasi ya kwanza katika madereva waliojiandikisha kushiriki mashindano ya Afrika.

Ushindi wake wa hivi punde nchini Uganda umemfanya kuzoa alama 201 zikisalia duru mbili za mwisho zitakazofanyika nchini Tanzania mnamo Septemba 13-15 na Rwanda mnamo Oktoba 4-6.

Kabla ya mataji matatu mfululizo kutoka kwa Baryan, Wakenya Jaspreet Chatthe na Don Smith walitawala mwaka 2015 na 2016 wakiendesha magari ya aina ya Mitsubishi na Subaru, mtawalia.

Madereva wengine kutoka Kenya waliowahi kuibuka mabingwa wa Afrika ni Shekhar Mehta aliyebeba taji la makala ya kwanza mwaka 1981 akipeleka gari la Nissan naye David Horsey aling’ara mwaka 1984 katika gari la Peugeot.