Basari: Magoha asuta wabunge kwa ubaguzi

Basari: Magoha asuta wabunge kwa ubaguzi

Na WINNIE ATIENO

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha, ameanzisha msako kuwatafuta wanafunzi ambao hawajajiunga na Kidato cha Kwanza huku akiwasuta baadhi ya wabunge kwa kutoa basari kwa ubaguzi.

Akizungumza Jumatatu katika Kaunti ya Mombasa, Prof Magoha aliwakashifu baadhi ya wabunge kwa ubaguzi wanapopeana basari kwa wanafunzi kupitia kwa Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maendeleo ya Maeneobunge (NG-CDF).

Katika ziara yake eneo bunge la Jomvu, waziri huyo alipata baadhi ya wanafunzi ambao walipita mtihani wa ya KCPE lakini hawajaenda shule za upili kwa kukosa karo.

“Ni vipi wanafunzi kama hawa ambao wanahitaji na wanafaa kupewa basari wananyimwa? Hii si haki. Mtoto anakaa nyumbani kwa sababu ya karo na kuna CDF? Tuache ubaguzi, watoto wote ni wetu, na watoto wote ni wa serikali. Hii tabia ya wanasiasa kupeana basari kibaguzi ikome. Najua wengine huwapa wale ambao ni wapiga kura wao,” akasema.

Wasimamizi wa CDF katika eneobunge la Jomvu akiwemo Bw Hamza Kombo, ambaye ni msaidizi wa Mbunge wa Jomvu Badi Twalib, walikuwa na wakati mgumu kujitetea namna wanafunzi wawili waliopita KCPE walivyokosa basari ya CDF.Wawili hao, Moses Shindani na mwenzake Biosa Hassan, walipata alama 394 na 355 mtawalia lakini kufikia Jumatatu, walikuwa hawajaenda shuleni kwa sababu ya matatizo ya kifedha katika familia zao.

Moses aliitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Butula, naye Biosa akaitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Moi Forces iliyo katika eneo la Mtongwe.

“Aliishiwa na matumaini kwa sababu ya uchochole, sisi kama wazazi hatukuwa na uwezo. Sina kazi, nina watoto watatu wengine shule ya upili lakini mmoja ilibidi aache kusoma,” alisema Bw Alvayo Shindani, babake Moses.

Mvulana huyo alisomea shule ya msingi ya kibinafsi ya Bethsaida eneo la Mikindani kupitia kwa ufadhili.

Bw Kombo alitetea wasimamizi wa CDF Jomvu akisema kuwa wanafunzi hao wawili ni miongoni mwa waliokosa basari kwa vile hawakusoma katika shule za umma jinsi ilivyohitajika kabla mwanafunzi kupewa ufadhili.

“Wawili hao walikosa basari kwa sababu walisomea shule za kibinafsi,” alisema Bw Kombo.

Prof Magoha aliagiza wizara yake kuwasaka wanafunzi wote ili waende shuleni wakiwemo wale waliopachikwa mimba.Aliagiza Moses apelekwe katika Shule ya Upili ya Shimo la Tewa mara moja, naye Biosa akipelekwa katika Shule ya Upili ya Mama Ngina.

Walipelekwa katika shule hizo hata bila sare za shule, Prof Magoha akisisitiza hakuna mwanafunzi anayefaa kuwa nyumbani wakati masomo yanaendelea shuleni.

“Afadhali shule zijae kuliko watoto kusalia nyumbani. Nimesikitishwa na eneo la Pwani ambapo watoto wengi wangali wako nyumbani. Hata wale waliopata alama za chini, wote waende shuleni. Hata kama hauna sare ya shule nenda ukasome,” alisema waziri.

You can share this post!

WANGARI: Mabadiliko katika NHIF yawe ya kumfaidi mwananchi

Hasara kuu kongamano la magavana likifutiliwa mbali