Kimataifa

Bashir alimiliki ufunguo wa ‘chumba chenye mabilioni’

September 8th, 2019 2 min read

NA AFP

MSIMAMIZI wa afisi ya aliyekuwa Rais wa Sudan Omar al-Bashir jana alieleza mahakama kwamba kiongozi huyo ndiye alikuwa na ufunguo wa chumba ambacho kilitumika kuhifadhi mabilioni ya fedha.

Akitoa ushahidi kwenye kesi inayomkabili Bashir kuhusu ufisadi na kuhifadhi pesa za wizi zilizokuwa kwenye sarafu za kigeni, msimamizi huyo Yasser Basheer pia alifichua kwamba kiongozi huyo alimpa zaidi ya Sh1.1 bilioni pesa taslimu wakati wa siku za mwisho za utawala wake ili kuwakabidhi watu mbalimbali mashuhuri.

Bashir aliondolewa madarakani mwezi Aprili mwaka huu baada ya misururu ya maandamano ya raia waliopinga utawala wake wa kidikteta. Kushtakiwa kwake hata hivyo kumetajwa na wachanganuzi kama kipimo halisi cha namna serikali mpya ya mpito itakavyohakikisha raia waliodhulumiwa wakati wa kipindi cha miaka 30 cha utawala wa Bashir wanapata haki.

Yasser ambaye alifanya kazi katika makazi ya Bashir kuanzia Septemba 2018, alifunguka zaidi na kusema kiongozi huyo aliwahi kumpa Sh573 Milioni ili amkabidhi Abdelrahim Hamdan Dagalo ambaye alikuwa Naibu Mkuu wa kikosi hatari cha kitengo cha jeshi(RSF).

Msimamizi huyo alisema pesa hizo ziliwasilishwa kwa Abdelrahim mbele ya nduguye Mohamed Hamdan Dagalo ambaye alikuwa mkuu wa RSF na Naibu Mkuu wa Baraza la Mpito la Jeshi(TMC) lililoongoza baada ya Bashir kuondolewa madarakani. Dagalo sasa ni mwanachama wa Baraza tawala linalowajumuisha wanajeshi na raia.

Kulingana na Yasser wengine waliopokezwa mabunda ya noti na Bashir ni maafisa wa wizara ya Ulinzi, wakuu wa jeshi na raia, pesa ambazo zilifaa kugharimia matibabu yao. Hata hivyo, alikanusha kwamba alifahamu kulikotoka pesa hizo, akieleza mahakama kwamba alikuwa akifuatwa tu amri ya mkubwa wake.

Shahidi mwengine Abdelmoneim Mohamed ambaye ni mhasibu katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika, pia alieleza korti kwamba chuo hicho kilipokea Sh458 milioni kutoka kwa Bashir.

Ingawa Bashir ambaye alikuwa korti akiwa amevaa mavazi ya kitamaduni ya rangi nyeupe hakuzungumza, alikanusha mashtaka hayo kortini juma lililopita.

Bashir alikiri kwamba alipokea Sh2.5 bilioni kutoka kwa mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman na watu wengine lakini akakanusha kwamba alitumia fedha hizo kujinufaisha.

Iwapo atapatikana na hatia kutokana na mashtaka mazito yanayomkabili, Bashir huenda akafungwa kwa muda usiopungua miaka 10 gerezani. Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea kusikizwa Septemba 14.