Michezo

Bashir: Utovu wa nidhamu ni hatari kwa soka

April 16th, 2019 1 min read

NA JOHN KIMWERE

KINARA wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Tawi la Nairobi West, Bashir Hussein amewataka wachezaji wa klabu zote chini ya tawi hilo wajiepushe na utovu wa nidhamu ili kufanikisha azimio lao katika soka.

”Vijana wanaolenga kubobea michezoni lazima waonyeshe nidhamu nzuri nyakati zote ndani pia nje ya Uwanja,” alisema na kuongeza kuwa waamuzi wote wanaume na wanawake wapaswa kuheshimiwa na kuachiwa kutekeleza majukumu yao hasa kusimamia mechi za soka kwa mujibu wa sheria husika.

Bashir alidokeza hayo alipokemea visa vya utovu wa nidhamu vilivyoshuhudiwa wikendi kwenye mechi tatu tofauti. Katika kisa cha kwanza, kwenye fainali za Chapa Dimba na Safaricom Season Two, mwamuzi wa kike, Eunice Ojiambo alivamiwa na wachezaji wawili wa Vapor Sports na kuvunjiwa miwani yake machoni walipompiga kwa mpira kumwadhibu wakidai alipendelea wapinzani wao waliyoibuka na ushindi.

Kisa cha pili kwenye mechi ya Ligi ya Kaunti, wafuasi wa Kuwinda United walishambulia mwamuzi wa katikati, Leonard Otundo kwa makonde wakilalamikia kutowajibika. Ofisa huyo alisema visa vya utovu vimo miongoni mwa wachezaji wachache baada ya kusaulika kwa muda.

Kisa cha tatu kwenye mchezo wa Nairobi West Regional League (NWRL), baina ya Lions na Makombora ambapo uliisha sare ya bao 1-1, ilidaiwa wafuasi wa Makombora walitishia mwamuzi wa katikati baada ya kumlisha kadi nyekundu mchezaji wa klabu hiyo.

Katika mpango mzima, mwenyekiti anasema watakutanishwa wafuasi na maofisa wa timu husika kutaka kufahamu kinachochagia kuibuka kwa tabia hiyo.