Habari

Bastola, risasi kadhaa zapatikana katika supamaketi Thika

January 10th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

POLISI wa Thika wanawasaka washukiwa wawili wanawake ambao waliacha kifurushi kilichokuwa na bastola na risasi kadhaa katika dukakuu la Naivas.

Kulingana na maelezo ni kwamba kifurushi hicho kimekuwa katika eneo la kuweka mizigo kwa zaidi ya siku 10 sasa, na ni mnamo Alhamisi Januari 9, 2020, ndipo walilazimika kufika hapo na kukifungua.

Afisa mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Thika, Bi Beatrice Kiraguri, alisema walijulishwa kuhusu jambo hilo na wasimamizi wakuu wa duka hilo la Naivas na ndipo wakafika kushuhudia.

Kulingana na afisa huyo, baada ya kukifungua kifurushi hicho – mfuko – walipata bastola, kipakatalishi, na risasi 40.

Matukio yaliyonaswa kwenye kamera ya CCTV yameonyesha wanawake wawili wakiingia ndani ya duka hilo na pia wakitoka huku polisi wakifuatilia tukio hilo.

Inadaiwa kuwa washukiwa hao ambao hawajanaswa waliiba bastola hiyo na bidhaa zingine kutoka kwa jamaa fulani eneo la Kandara mnamo Disemba 30, 2019. Na mwenye mali hiyo alikuwa mazishini na bastola hiyo ilitolewa kwenye gari lake.

Baada ya kifurushi hicho kuwa eneo hilo la mizigo kwa muda mrefu, wafanyakazi wa hapo walishuku na kuarifu wakubwa wao ambao pia walichukua hatua ya haraka na kueleza polisi.

Baadaye mmiliki wa bastola hiyo alipiga ripoti katika kituo cha Polisi cha Kandara kaunti ya Murang’a, ambapo uchunguzi ulianza kufanywa.

Kulingana na wafanyi kazi wa duka hilo la jumla ilidaiwa wanawake wawili walifika eneo hilo na kifurushi kilichokuwa ndani ya mfuko na kuliacha eneo la kuachia mizigo.

Baada ya wao kuingia mle dukani, walimaliza dakika chache na kutoweka bila kuchukua mzigo wao.

Meneja mkuu wa duka hilo Bw Daniel Mukuha alisema hata wao walishangazwa na kitendo hicho ambapo bado wanatafakari jinsi tukio hilo lilijiri.

“Sisi kama kawaida haturuhusiwi kupekua mali ya mteja yeyote lakini baada ya mfuko huo kupatikana mahali hapo kwa muda, tuliona vyema kuarifu Polisi,” alisema Bw Mukuha.

Alisema tayari wamekuwa kwenye kikao cha dharura kama kampuni ili kujadili kwa kina hali ya usalama na njia mwafaka wa kuchukua baada ya tukio hilo.

Alieleza kuwa watazidi kupiga doria kali ili kukabiliana na utovu wa usalama jinsi  inavyostahili. Hata wateja wanastahili kuarifiwa na kuhamasishwa kuhusu maswala ya usalama.