Habari Mseto

Bastola ya polisi yaibwa akioga

March 31st, 2019 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

MAAFISA wa Idara ya upelezi wa jinai (DCI), Kaunti ya Murang’a, wanachunguza tukio ambapo silaha ya afisa wa kitengo hicho ilipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Silaha hiyo, bastola aina ya Ceska, iliyokuwa na risasi ilisemekana kuibwa kutoka nyumba ya afisa huyo wiki hii.

Wapelelezi wana kibarua cha kufumbua nani aliweza kuingia katika nyumba hiyo kwenye makazi ya maafisa wa usalama na kuiba bastola hiyo.

Mkuu wa upelelezi eneo la Murang’a Mashariki (DCIO), Juliana Muthini, alisema mmoja wa maafisa wake aliripoti katika afisi yake kuwa bunduki hiyo iliibwa Jumanne asubuhi.

Alisema afisa huyo anaishi peke yake katika nyumba za makazi za polisi na wachunguzi wanajaribu kufuatilia matukio yaliyopelekea bunduki hiyo kupotea.

“Tuko karibu kukamilisha uchunguzi ambapo tutaeleza tutakachobaini na kutuma faili kwa idara zifaazo kwa ushauri zaidi,” Bi Muthini alieleza Taifa Jumapili.