Habari Mseto

Bastola zaibwa polisi wakishabikia mechi

April 17th, 2019 1 min read

NA TOM MATOKE

BASTOLA tatu aina ya G3 zilizokuwa na risasi 20, Jumanne usiku ziliibwa katika Kituo cha Polisi wa Utawala cha Aldai, Kaunti ya Nandi, maafisa wanaohudumu kituoni humo, walipoenda kutazama mechi za soka.

Polisi hao waliripotiwa kutoka kituoni humo hadi kituo cha kibiashara cha Chepturo, karibu na Chuo cha Walimu cha Kaimosi ili kutazama mechi za Klabu Bingwa Barani Ulaya(UEFA), kati ya Barcelona na Manchester United na vile vile Juventus dhidi ya Ajax.

Chepturo inapatikana umbali wa kilomita nne kutoka kituo hicho cha polisi.Hata hivyo, walipata pigo jingine baada ya timu walizokuwa wakishabikia za Manchester United na Juventus kubanduliwa nje ya kipute hicho na kusitisha ndoto zao za kutinga nusu fainali.

Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Nandi, Bw Samuel Kimiti, ametangaza kwamba wameanzisha oparesheni kali wakisaidiana na maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Uhalifu wa Jinai ili kutafuta silaha hizo.