Habari Mseto

Bawabu auawa kwenye wizi wa mabavu

August 26th, 2020 1 min read

NA GEORGE MUNENE

Bawabu mmoja amekatakatwa hadi kifo huku mwingine akijeruhiwa vibaya kwenye wizi wa mabavu uliofanyika kwenye soko la Kathageri, Kaunti ya Embu.

Aliyejehuriwa alikimbizwa katika hospitali ya Runyenjes na kulazwa akiwa hali mahututi. Wakazi waliojawa na ghadhabu waliandamana Jumatatu asubuhi kukemea kitendo hicho.

Mabawabu hao walikuwa wanalinda duka linalomilikiwa na mkazi mmoja wakati majambazi hao walifika  saa tisa usiku Jumatatu na kuwavamia.

Hapo ndipo walikabiliana na wao na kwa bahati mbaya wakashindwa nguvu na majambazi hao na mmoja akauwawa papo hapo na mwingine akaumizwa.

Kulingana na wakazi, wahuni hao walivamia duka hilo na  kuiba unga wa mahindi, sukari, nguo, viatu na bidhaa zingine za thamani ya maelfu.

Tukio hilo lilitendeka mita chache kutoka kituo cha polisi cha Kathangeri.

Wakazi na wafanyabiashara waliotikia kilio hicho walipata bawabu huyo aliyeumizwa akiwa amekatwa kichwani huku akiwa na mauvimu mengi na wakampeleka hospitali.

Kutokana na mavamizi hayo wakazi waliandamana kufuatia kuongozeka kwa utovu wa usalama eneo hilo. Walikatiza shughuli za uchukuzi huku wakiwalaumu polisi kwa kuzebea kazini  mwao.

TAFSIRI: FAUSTINE NGILA