Michezo

Bayer 04 Leverkusen ni miongoni mwa klabu zinazowania huduma za Wanyama

January 31st, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAYER Leverkusen (Ujerumani), Fiorentina na Lazio (Italia) na Rennes na Strasbourg (Ufaransa) zimejitosa uwanjani kuwania huduma za Mkenya Victor Mugubi Wanyama, ambaye Tottenham Hotspur inatarajiwa kuruhusu aondoke kabla ya kipindi kifupi cha uhamisho kifungwe Januari 31 saa tano usiku saa za Uingereza.

Norwich, Aston Villa na West Ham (Uingereza), Celtic (Scotland) na Galatasaray (Uturuki) pia zilihusishwa na Wanyama mara tu soko la Januari lilifunguliwa Januari 1, 2020.

Katika kipindi hiki, fununu pia zilisema Lyon (Ufaransa), AC Milan (Italia) na Hertha Berlin (Ujerumani) zinamezea mate nahodha huyo wa timu ya taifa ya Kenya ya Harambee Stars.

Ripoti zimesema Ijumaa kuwa Tottenham sasa imepunguza bei ya Wanyama kutoka Sh1.2 bilioni hadi Sh1.0 bilioni. Ilitaka kuuza Wanyama kwa Sh2.2 bilioni katika kipindi kirefu cha uhamisho kilichopita, huku bei hiyo ikiteremka hadi 1.7 bilioni kabla ya kiungo huyo kukataa kujiunga na Club Brugge nchini Ubelgiji mapema Septemba mwaka 2019.

Ikisalia miezi 18 kandarasi ya Wanyama katika klabu ya Tottenham ikatike, Tottenham inaaminika iko tayari kuruhusu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 aondoke hata kwa mkopo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy ametoa masharti kwa klabu inayotaka Wanyama kwa mkopo. Vyombo vya habari nchini Uingereza vinasema kuwa Levy ameitisha ada ya Sh198 milioni na pia kujumuishwa kwa kipengee katika makubaliano hayo kinacholazimisha klabu inayomchukua kwa mkopo imnunue kabisa mwisho wa msimu.

Aidha, ripoti nchini Uingereza zinadai kuwa Wanyama hajakuwa makini kujiunga na klabu zinazommezea mate barani Ulaya kwa sababu mwenyewe anatamani kuajiriwa na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu nchini Amerika (MLS).

Hata hivyo, inasemekana mshahara mkubwa wa Sh8.5 milioni anaopokea Spurs umekuwa kisiki kwa klabu za MLS kumtafuta. Haziko tayari kumlipa kiasi hicho cha fedha.

Wanyama alijiunga na Tottenham kwa Sh1.4 bilioni kutoka Southampton mwaka 2016 na alikuwa tegemeo.

Aliichezea mechi 47 na kupachika mabao matano, lakini majeraha yamemsumbua kiasi cha Tottenham kumuona kuwa mzigo kwa klabu hiyo. Amechezeshwa dakika chache katika mechi nne pekee msimu huu, huku kocha Jose Mourinho akiamua kumuacha nje ya mipango yake.