Michezo

Bayern kukosa huduma za Neuer kwa majuma mawili

April 15th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MABINGWA watetezi wa Ligi ya Ujerumami (Bundesliga) Bayern Munich, watazikosa kwa muda wa wiki mbili huduma za nyani wao mahiri Manuel Neuer ambaye aliumia wakati wa mechi ya ligi dhidi ya Fortuna Dusseldorf.

Neuer ambaye ni nohadha wa Bayern Munich alitonesha jeraha kwenye goti lake baada ya kuliumiza kwenye mechi za ligi dhidi ya Freiburg na Heidenheim na sasa huenda akakosa mechi mbili kati ya tano zilizosalia kabla ligi haijakamilika.

Bayern Munich wanaonolewa na Niko Kovac wapo kileleni mwa msimamo wa jedwali, alama moja mbele ya nambari mbili Borussia Dortmund na watakutana na Werder Bremen nyumbani kabla ya kuvaana na Nurnberg ugenini. Pia wana kibarua kigumu dhidi ya Werder Bremen kwenye Kombe la DFB-Pokal.

Mlinzi wa Bayern Mats Hummels pia anakabiliwa na jeraha baada ya kuumia wakati wa ushindi wa 4-1 dhidi ya Fortuna Dusseldorf huku ikibainika atakosa mazoezi kwa kipindi kifupi hadi hali yake iimarike.

Bayern wapo mbioni kutwaa Bundesliga kwa mwaka wa saba mfululizo baada ya mabao mawili ya Kingsley Coman na mengine yaliyofungwa na Serge Gnabry na Leon Goretzka kuwapa ushindi dhidi ya Fortuna Dusseldorf.

Wakati uo huo Kovac ameisifu timu yake kwa kunyeshea Borussia Dortmund mabao 5-0 mnamo Aprili 6, 2019, matokeo yaliyowapaisha hadi kileleni mwa jedwali.

“Tulikuwa makini kwa dakika 90 na hatukuwapa nafasi watufunge. Ulikuwa ushindi mtamu na hatutakubali kubanduka usukani tena,” akasema Kovac.