Michezo

Bayern Munich bado kileleni mwa jedwali la Bundesliga licha ya kuambulia sare na Werder Bremen

November 22nd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LICHA ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Werder Bremen kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), Bayern Munich walisalia kileleni mwa jedwali kwa alama 19, moja zaidi kuliko wapinzani wao wakuu, Borussia Dortmund.

Maxi Eggestein aliwaweka Werder uongozini mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya fowadi raia wa Ufaransa, Kingsley Coman kusawazisha mambo katika dakika ya 62 baada ya kushirikiana na kiungo Leon Goretzka.

Bayer Leverkusen walichupa hadi nafasi ya pili na kupunguza pengo la alama kati yao na Bayern hadi pointi moja pekee baada ya kuwapepeta limbukeni Arminia Bielefeld 2-1 ugenini.

Kipa Manuel Neuer alifanya kazi ya ziada na kuwanyima wavamizi wa Werder – Josh Sargent na Ludwig Augustinsson nafasi mbili za wazi ambazo vinginevyo zingalifanya mambo kuwa 3-0 mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Sargent alihusika pia katika bao la kwanza ambalo Werder walifungiwa na Eggestein.

Ingawa Bayern walitamalaki kipindi cha pili cha mchuano huo, juhudi zao hazikuzalisha matunda huku makombora mawili ya fowadi Douglas Costa yakigongwa mwamba wa goli la wapinzani wao.

Baada ya Coman kusawazisha mambo, Bayern walipata nafasi mbili za kujiweka uongozini ila wachezaji Eric Maxim Choupo-Moting na Leroy Sane wakapaisha mpira licha ya kusalia uso kwa macho na kipa wa Werder waliokuwa wakichezea ugenini.

Matokeo hayo yaliwasaza Werder katika nafasi ya tisa kwa alama 11 sawa na Stuttgart, Augsburg na Eintracht Frankfurt.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Novemba 21, 2020):

Bayern Munich 1-1 Werder Bremen

Hertha Berlin 2-5 Borussia Dortmund

M’gladbach 1-1 Augsburg

Arminia 1-2 Leverkusen

Schalke 0-2 Wolfsburg

Hoffenheim 3-3 Stuttgart

Frankfurt 1-1 RB Leipzig