Michezo

Bayern Munich wapiga wenyeji Borussia Dortmund 1-0

May 26th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAYERN Munich walianza kunusia ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mara ya nane mfululizo msimu huu baada ya kuwazamisha Borussia Dortmund 1-0 uwanjani Signal Park Iduna.

Wakinolewa na kocha wa sasa wa Liverpool, Jurgen Klopp, Dortmund walitawazwa mabingwa wa Bundesliga mnamo 2010-11 na 2011-12.

Tangu wakati huo, Bayern wamekuwa wakijivunia ukiritimba mkubwa katika soka ya Ujerumani.

Bao lililowavunia Bayern alama tatu katika gozi dhidi ya Dortmund lilifumwa wavuni na Joshua Kimmich aliyemwacha hoi kipa Roman Burki kunako dakika ya 43.

Baada ya kuonekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara, Dortmund walilazimika kumleta ugani chipukizi Jadon Sancho katika kipindi cha pili ila ujio wake haukutosha kuwarejesha waajiri wake mchezoni.

Ushindi wa Bayern uliwasaza kileleni mwa jedwali la Bundesliga kwa alama 64, saba zaidi kuliko Dortmund wanaoshikilia nafasi ya pili huku zikisalia mechi sita pekee kwa kampeni za msimu huu kutamatika rasmi.

Nusura mshambuliaji Robert Lewandowski awafungie Bayern bao la pili mwishoni mwa kipindi cha pili ila akashuhudia kombora lake kutoka eneo la penalti likibusu mwamba wa goli la Dortmund.

Kabla ya mchuano huo kutandazwa, Lewandowski na chipukizi Erling Braut Haaland wa Dortmund ndio waliopigiwa upatu wa kutamba zaidi ugani na kuzolea waajiri wao ushindi.

Wawili hao wanajivunia kufunga jumla ya mabao 41 kutokana na mechi 35 zilizopita, ufanisi unaowaweka kileleni mwa orodha ya wafungaji bora katika soka ya bara Ulaya.

Haaland alikaribia kutia kapuni bao lake la 42 chini ya kipindi cha sekunde 35 za mwanzo wa kipindi wa kwanza baada ya kumzidi maarifa kila Manuel Neuer aliyekuwa akinogesha mchuano wake wa 400 katika soka ya Bundesliga. Hata hivyo, juhudi za Haaland ambaye ni mzawa wa Norway, zilizimwa na beki Jerome Boateng.

Ingawa Thorgan Hazard alicheka na nyavu za Bayern, goli lake la dakika ya 67 halikuhesabiwa na refa kwa madai kwamba lilifungwa akiwa ameotea.

Ushindi wa Bayern uliendeleza rekodi yao ya kutoangushwa na kikosi chochote katika jumla ya mechi 18 zilizopita tangu wapokezwe kichapo cha 2-1 kutoka kwa Borussia Monchengladbach mnamo Disemba 7, 2019.

Bayern ambao pia wametinga nusu-fainali za German Cup, wanajivunia kuwapepeta Chelsea 3-0 katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Miamba hao wa soka ya Ujerumani kwa sasa wamesajili ushindi katika jumla ya mechi 21 kutokana na 24 zilizopita chini ya kocha mpya Hansi Flick aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Niko Kovac aliyetimuliwa Novemba 2019 Bayern wakishikilia nafasi ya nne jedwalini.