Bayern Munich waponda Bochum na kufikisha mabao 20 kutokana na mechi tano za Bundesliga

Na MASHIRIKA

BAYERN Munich waliponda limbukeni VfL Bochum 7-0 katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Jumamosi.

Joshua Kimmich alifungia Bayern mabao mawili baada ya kiungo mvamizi Leroy Sane kufungua karamu ya magoli kupitia mpira wa ikabu.Serge Gnabry, Robert Lewandowski na Eric Maxim Choupo-Moting walikuwa wafungaji wa mabao mengine ya Bayern baada ya Vasilis Lampropoulos wa Bochum kujifunga.

Bayern walisakata mechi hiyo wakiwa wamevalia jezi za rangi ya kijani kibichi iliyokolea ambayo ni yao ya nne muhula huu.Bayern walikuwa wamejipa uhakika wa kuibuka washindi wa mechi hiyo kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza baada ya Lampropoulos kujifunga na kufanya mambo kuwa 4-0 ugani Allianz Arena.

Ushindi huo wa Bayern sasa unafanya mabao yao kufikia 20 kutokana na mechi tano pekee za ufunguzi wa msimu huu.