Bayern Munich waponda Viktoria Plzen nchini Ujerumani na kuendeleza ubabe wao katika UEFA

Bayern Munich waponda Viktoria Plzen nchini Ujerumani na kuendeleza ubabe wao katika UEFA

Na MASHIRIKA

BAYERN Munich waliendeleza ubabe wao katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa kuponda Viktoria Plzen ya Jamhuri ya Czech 5-0 katika mechi ya Kundi C mnamo Jumanne.

Leroy Sane, Serge Gnabry na Sadio Mane walifungia Bayern chini ya dakika 21 za ufunguzi wa kipindi cha kwanza na kurahisisha kazi ya kikosi chao kilichofungua kampeni za Kundi C kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Inter Milan kabla ya kupokeza Barcelona kichapo sawa na hicho.

Sane alipachikwa wavuni bao la nne la Bayern kabla ya Eric-Maxim Choupo-Moting kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao uwanjani Allianz Arena.

Matokeo hayo yalisaza Bayern kileleni mwa Kundi C kwa alama tisa kutokana na mechi tatu. Maandalizi ya mechi hiyo kwa upande wa Bayern yalivurugwa kiasi baada ya Joshua Kimmich na Thomas Muller kuachwa nje baada ya vipimo vya afya kubaini kuwa walikuwa wakiugua Covid-19.

Jamal Musiala aliyeshirikiana vilivyo na mafowadi wa Bayern alishuhudia bao lake likifutiliwa mbali baada ya teknolojia ya VAR kubaini kuwa alikuwa ameotea.

Sane ambaye ni fowadi wa zamani wa Manchester City, sasa ana mabao manne kutokana na mechi nne za UEFA muhula huu.

Licha ya kutamba katika UEFA, kipute wanachopigiwa upatu wa kunyanyua muhula huu, Bayern wanasuasua katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) chini ya kocha Julian Nagelsmann. Kufikia sasa, wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini nyuma ya Union Berlin na SC Freiburg.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Uhalalishaji wa GMO wazua mjadala mkali

Mhariri asukumwa ndani kwa kudharau mahakama

T L