Bayern Munich watia kapuni taji la Bundesliga kwa mara ya tisa mfululizo

Bayern Munich watia kapuni taji la Bundesliga kwa mara ya tisa mfululizo

Na MASHIRIKA

BAYERN Munich walisherehekea kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa msimu wa tisa mfululizo kwa kuwapepeta Borussia Monchengladbach 6-0 mnamo Jumamosi.

Bayern waliingia ugani kwa ajili ya mchuano huo wakiwa tayari wamehakikishiwa ubingwa baada ya nambari mbili RB Leipzig kupigwa 3-2 na Borussia Dortmund katika gozi la awali.

Magoli mawili kutoka kwa kigogo Robert Lewandowski, Thomas Muller na Kingsley Coman yalivunia Bayern uongozi wa 4-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.

Lewandowski aliyefunga jumla ya magoli matatu katika mchuano huo alipachika waajiri wake bao la tatu kupitia penalti katika dakika ya 65 kabla ya kiungo wa zamani wa Manchester City, Leroy Sane, kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao mwishoni mwa kipindi cha pili.

Chini ya kocha Hansi Flick, Bayern walikamilisha pambano hilo wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya chipukizi Tanguy Nianzou aliyeletwa ugani katika kipindi cha pili kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 75.

Leipzig walioanza mechi wakiwa na kiu ya kupunguza pengo la alama saba lililokuwa likitamalaki kati yao na Bayern walizidiwa maarifa na Dortmund ambao kwa sasa wanakamata nafasi ya nne kwa alama 58, mbili nyuma ya VfL Wolfsburg wanaoshikilia nafasi ya tatu. Zimesalia mechi tatu pekee kwa kampeni za Bundesliga msimu huu kutamatika rasmi.

Mwingereza Jadon Sancho aliwafungia Dortmund goli la pili baada ya Marco Reus kufungua ukurasa wa mabao. Ingawa Lukas Klostermann na Dani Olmo walisawazishia Leipzig, Sancho alizamisha chombo cha wageni wao katika tukio lililowavunia Bayern taji la Bundesliga kabla ya hata kushuka dimbani kumenyana na Monchengladbach.

Ushindi wa Dortmund uliwaweka hai matumaini yao ya kukamilisha kampeni za Bundesliga msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na hatimaye kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Mnamo Aprili, Bayern walitangaza kuwa kocha Julian Nageslmann wa Leipzig ataanza kudhibiti mikoba yao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo baada ya mkufunzi Hansi Flick kufichua mipango ya kuagana na miamba hao wa Bundesliga.

Flick anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kupokezwa mikoba ya timu ya taifa ya Ujerumani baada ya kocha Joachim Loew kuagana na mabingwa hao wa zamani wa dunia mnamo Julai baada ya fainali za Euro 2021 kukamilika.

Kocha raia wa Amerika, Jesse Marsch, ambaye kwa sasa anawatia makali masogora wa RB Salzburg katika Ligi Kuu ya Austria, ndiye atapokezwa chombo cha Leipzig baada ya Nagelsmann kuondoka mwishoni mwa muhula huu.

Kwingineko, kocha Edin Terzic anashikilia tu mikoba ya Dortmund kwa muda na nafasi yake itatwaliwa rasmi na mkufunzi Marco Rose wa Monchengladbach mwishoni mwa muhula huu.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Jumamosi):

Dortmund 3-2 Leipzig

Bayern 6-0 M’gladbach

Bremen 0-0 Leverkusen

Hoffenheim 4-2 Schalke

Wolfsburg 3-0 Union Berlin

You can share this post!

Maandamano yaendelea Chad wiki kadhaa baada ya kifo cha...

Manchester City kusubiri zaidi kutwaa taji la EPL baada ya...