Bayern Munich yadengua Al Ahly na kufuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Tigres UANL ya Mexico

Bayern Munich yadengua Al Ahly na kufuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Tigres UANL ya Mexico

Na MASHIRIKA

ROBERT Lewandowski alifunga mabao mawili dhidi ya Al Ahly ya Misri na kusaidia Bayern Munich kufuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia kwa Klabu (Fifa Club World Cup) nchini Qatar.

Bayern ambao ni miamba wa soka ya Ujerumani na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), walitamalaki mchezo katika kipindi cha kwanza na kumiliki asilimia kubwa ya mpira.

Kikosi hicho cha kocha Hansi Flick kiliwekwa uongozini na Lewandowski katika dakika ya 17 kabla ya nahodha huyo wa timu ya taifa ya Poland kufuma la pili mwishoni mwa kipindi cha pili. Goli la Lewandowski lilikuwa lake la 29 kutokana na mechi 27 ambazo amechezea Bayern hadi kufikia sasa msimu huu.

Al Ahly walijituma zaidi katika kipindi cha pili japo kasi yao haikuzalisha matunda. Al Ahly wana uzoefu na tajriba pevu kwenye Kombe la Dunia baada ya kunogesha fainali za Kombe la Dunia mnamo 2005, 2006, 2008, 2012 na 2013.

Walifuzu kwa kivumbi cha mwaka huu baada ya kutandika Zamalek SC ambao ni watani wao katika Ligi Kuu ya Misri 2-1 kwenye fainali ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) mnamo Novemba 2020.

Bayern kwa sasa watavaana na Tigres UANL ya Mexico kwenye fainali itakayosakatiwa nchini Qatar mnamo Alhamisi ya Februari 11, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Sonko apelekwa kortini kwa ambulensi

Vyakula vya kiamsha kinywa kwa ajili ya kupunguza uzani