Bayern Munich wanyanyasa Cologne na kuendeleza ubabe wao Bundesliga

Bayern Munich wanyanyasa Cologne na kuendeleza ubabe wao Bundesliga

Na MASHIRIKA

ROBERT Lewandowski na Serge Gnabry walifunga mabao mawili kila mmoja na kusaidia Bayern Munich kuendelea kudhibiti kilele cha jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) baada ya kupepeta Cologne 5-1 mnamo Jumamosi.

Eric Maxim Choupo-Moting alifungulia Bayern ukurasa wa mabao katika dakika ya 18 kabla ya Lewandowski kufunga la pili baada ya kukamilisha krosi ya kiungo Leon Goretzka.

Ingawa Ellyes Skhiri aliwarejesha Cologne mchezoni katika dakika ya 49, Thomas Muller alichangia bao la pili la Lewandowski na kuwarejeshea Bayern uongozi wa mabao mawili.

Gnabry ambaye ni kiungo wa zamani wa Arsenal, alifunga mabao mawili ya haraka chini ya dakika 10 za mwisho wa kipindi cha pili na kuhakikisha kwamba waajiri wake wanaondoka ugani na magoli matano.

Ushindi huo uliwadumisha Bayern uongozini kwa alama 52, mbili zaidi kuliko nambari mbili RB Leipzig waliotoka nyuma na kukung’uta Borussia Monchengladbach 3-2 katika mechi nyingine ya Bundesliga.

Lewandowski ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland, sasa amefunga mabao 28 katika Bundesliga msimu huu wa 2020-21.

Zikisalia mechi 11 pekee kwa kampeni za msimu huu kutamatika rasmi, Lewandowski, 32, yuko mbioni kuvunja rekodi ya jagina Gerd Muller aliyewahi kufunga jumla ya mabao 40 katika msimu mmoja wa Bundesliga mnamo 1972.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Man-City wacharaza West Ham United na kuanza kunusia taji...

Mjane wa balozi wa Italia nchini DRC avunja kimya