Bayern waponda Schalke na kufungua mwanya wa alama saba kileleni mwa jedwali la Bundesliga

Bayern waponda Schalke na kufungua mwanya wa alama saba kileleni mwa jedwali la Bundesliga

Na MASHIRIKA

BAYERN Munich walifungua mwanya wa alama saba kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Jumapili baada ya kuwapokeza Schalke kichapo cha 4-0 ugenini.

Bayern walifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa kiungo Thomas Muller kunako dakika ya 33 kabla ya Robert Lewandowski kupachika wavuni bao la pili ambalo lilikuwa lake la nane mfululizo ligini.

Mabao mengine ya Bayern yalifumwa wavuni na Muller na David Alaba katika dakika za 88 na 90 mtawalia.

“Ingawa tulishinda kwa idadi kubwa ya mabao, sikuridhishwa na jinsi tulivyocheza mechi hiyo. Vijana walipoteza mipira mara kwa mara. Ipo haja kwa kikosi kuanza kumiliki asilimia kubwa ya mpira uwanjani na wachezaji kupokezana pasi za haraka,” akasema kocha wa Bayern, Hansi Flick.

Kiungo Joshua Kimmich wa Bayern alichangia mabao matatu yaliyofungwa na waajiri wake katika mchuano huo huku kipa Manuel Neuer ambaye pia ni chaguo la kwanza katika timu ya taifa ya Ujerumani akiweka rekodi ya kutofungwa kwenye jumla ya mechi 197 za Bundesliga.

Ushindi dhidi ya Schalke uliwaweka Bayern pazuri zaidi kadri wanavyowania fursa kutia kapuni taji la Bundesliga kwa mara ya tisa mfululizo.

Nambari mbili RB Leipzig walipoteza fursa ya kupunguza pengo la alama kati yao na Bayern baada ya kupigwa 3-2 na Mainz katika mechi nyingine ya Bundesliga.

Leipzig kwa sasa wanajivunia alama 35, tatu zaidi kuliko Bayer Leverkusen na VfL Wolfsburg wanaoshikilia nafasi za tatu na nne mtawalia.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Januari 24):

Schalke 0-4 Bayern

Hoffenheim 3-0 FC Koln

You can share this post!

AC Milan wamsajili fowadi matata raia wa Croatia, Mario...

Leicester wakomoa Brentford na kujikatika tiketi ya kuvaana...