Michezo

Bayern wazidi kufuka moto Bundesliga

May 23rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAYERN Munich watashuka dimbani kuvaana na Borussia Dortmund katika gozi la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Jumanne ya Mei 26, 2020 wakijivunia pengo la alama nne kileleni mwa jedwali.

Hii ni baada ya miamba hao wa soka ya Ujerumani kuwapepeta Eintracht Frankfurt 5-2 katika mchuano uliowakutanisha ugani Allianz Arena.

Bayern ya kocha Hansi Flick sasa wametia kapuni alama 61 kutokana na mechi 27 zilizopita.

Bayer Leverkusen walipaa hadi nafasi ya tatu kwa alama 53 baada ya kuwapokeza Borussia Monchengladbach wanaofunga mduara wa nne kwa alama 52 kichapo cha 3-1.

Bayern walijibwaga ugani dhidi ya Frankfurt wakiwa na ulazima wa kusajili ushindi ili kuepuka presha kutoka kwa Dortmund waliovuna ushindi wa 2-0 dhidi ya VfL Wolfsburg.

Leon Goretzka aliwafungulia Bayern ukurasa wa mabao kunako dakika ya 17 kabla ya Thomas Muller kupachika wavuni la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Robert Lewandowski aliyafanya mambo kuwa 3-0 mwanzoni mwa kipindi cha pili dakika chache kabla ya beki Martin Hinteregger aliyefunga magoli mawili ya haraka kunako dakika ya 52 na 55 kabla ya kujifunga mwishoni mwa kipindi cha pili kuwarejesha Frankfurt mchezoni.

Bao jingine la Bayern ambao wanapania kutetea ubingwa wao wa taji la Bundesliga muhula huu lilifumwa wavuni na Alphonso Davies kunako dakika ya 61.

Ushindi wa Bayern una maana kwamba Frankfurt kwa sasa wamepoteza jumla ya mechi tano mfululizo na wamefungwa mabao matano katika michuano miwili iliyowakutanisha na Bayern muhula huu.

Bao la Lewandowski lilikuwa lake la 41 kutokana na mechi 35 ambazo amechezea Bayern katika michuano yote hadi kufikia sasa msimu huu. Kivumbi cha Bundesliga kilianza upya mnamo Mei 16, 2020 huku wadau wote wakizingatia kanuni mpya za afya.

Kuahirishwa kwa kampeni za Bundesliga kulifanyika wakati ambapo Bayern walikuwa wakijivunia fomu nzuri iliyowawezesha kusajili ushindi mara 10 kutokana na jumla ya mechi 11 mfululizo.

Kabla ya kuvaana na Frankfurt, mchuano wao wa mwisho kutandaza katika Bundesliga ulikuwa dhidi ya Union Berlin waliopokea kichapo cha 2-0 wikendi iliyopita. Awali, walikuwa wamewatandika Chelsea 3-0 katika mkondo wa kwanza wa mwondoano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na kuwabandua Schalke kwenye robo-fainali za German Cup.

MATOKEO YA BUNDESLIGA

Bayern 5-2 Frankfurt

M’gladbach 1-3 Bayer Leverkusen

Paderborn 1-1 Hoffenheim

Freiburg 0-1 Werder Bremen

Wolfsburg 0-2 Dortmund

Hertha Berlin 4-0 Union Berlin