Michezo

Bayern yanusia ubingwa kwa mara ya 8 mfululizo

June 7th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAYERN Munich wanahitaji sasa kusajili ushindi mara mbili pekee kutokana na mechi nne zilizosalia msimu huu ili kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mara ya nane mfululizo.

Hii ni baada ya vijana hao wa kocha Hansi Flick kutoka nyuma na kuwazamisha Bayer Leverkusen kwa mabao 4-2 uwanjani Bay Arena.

Kingsley Coman, Leon Goretzka na Serge Gnabry walifunga mabao ya Bayern katika kipindi cha kwanza baada ya Lucas Alario kuwafungulia wenyeji Leverkusen ukurasa wa magoli.

Bao la Robert Lewandowski aliyetikisa nyavu za Leverkusen kunako dakika ya 66, lilikuwa lake la 30 katika kampeni za Bundesliga msimu huu ndani ya jezi za Bayern.

Bayern wamepoteza mechi mbili pekee kati ya 26 zilizopita chini ya Flick aliyeaminiwa fursa ya kumrithi Niko Kovac aliyetimuliwa Novemba 2019 kwa sababu ya matokeo duni.

Kibarua kifuatacho cha Bayern ni gozi la nusu-fainali ya German Cup litakalowakutanisha na Eintracht Frankfurt mnamo Juni 10, 2020.

Borussia Dortmund ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 63, saba nyuma ya Bayern walifaulu pia kuwazamisha Hertha Berlin 1-0 kupitia bao la Emre Can.

Leverkusen waliokosa huduma za mshambuliaji wao matata Kai Havertz walijibwaga ugani wakilenga kuendeleza rekodi ya kupoteza mechi moja pekee kati ya 14 za awali. Bao la kwanza walilofungiwa na Alario lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati ya fowadi huyo mzawa wa Argentina na kiungo Julian Baumgartlinger.

Tineja Florian Wirtz, 17, alitokea benchi katika kipindi cha pili na kuwafungia Leverkusen bao la pili kunako dakika ya 89 baada ya kumwacha hoi kipa Manuel Neuer.

Lewandowski ambaye anapigiwa upatu wa kuibuka mfungaji bora wa Bundesliga kwa mara nyingine msimu huu, atakosa mechi ya ligi dhidi ya Borussia Monchengladbach wikendi ijayo baada ya kuonyeshwa kadi ya manjano.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Poland kwa sasa anajivunia jumla ya mabao 44 kutokana na mapambano yote ambayo amewasakatia Bayern muhula huu. Sogora huyo ana mechi tatu pekee za ligi kupachika wavuni mabao 10 ili kufikia rekodi ya kigogo wa zamani wa Bayern, Gerd Muller aliyewahi kufunga magoli 40 katika msimu mmoja wa Bundesliga.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Juni 6):

Leverkusen 2-4 Bayern

Leipzig 1-1 Paderborn

Dortmund 1-0 Hertha Berlin

Frankfurt 0-2 Mainz

Dusseldorf 2-2 Hoffenheim