Michezo

Bayern yawapa aheri staa Ribery, Robben

May 22nd, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

MUNICH, Ujerumani

VIGOGO wa Ujerumani, Bayern Munich walimaliza ligi kuu ya Bundesliga kwa kishindo walipotwaa kombe hilo mbali na kuwaaga miamba na mihimili yao; Franck Ribery na Arjen Robben.

Vijana hao wa kocha Niko Kovac walinyakua taji hilo baada ya kuwanyuka Entracht Frankfurt mabao 5-1 na kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya saba mfululizo.

Mabingwa hao, kadhalika wanajiandaa kukutana na Leipzig katika fainali ya kuwania ubingwa wa Germany Cup kwenye mechi ambayo itachezwa mwishoni mwa wiki.

Ushindi huo umekuja wakati kuna uvumi kwamba huenda kocha Kovac akatimuliwa kufuatia madai ya kuvurugana na baadhi ya wachezaji, licha ya kuleta ufanisi huo hasa ikikumbukwa kwamba kufikia mwezi Desemba, timu hiyo ilikuwa nyuma ya Borussia Dortmund kwa tofauti ya pointi tisa.

Ushindi wao wa taji la Bundesliga uliandamana na sherehe za kuwaaga miamba watatu, Rafinha, 33, Robben, 35 na Ribery, 36 ambao kwa pamoja wameitumikia kwa miaka 30.

Washambuliaji wa pembeni

Robben na Ribery watakumbukwa zaidi ikizingatiwa kwamba baada ya kujiunga na klabu hiyo kama washambuliaji wa pembeni, hatimaye walibadilika na kuwa viungo mahiri enzi za kocha Pep Guardiola.

Hata hivyo, licha ya kuondoka kwa nyota hao pamoja na mabadiliko mengine yaliyofanywa, itabidi kocha Kovac aunde upya kikosi chake la si hivyo, taji la msimu ujao halitakuwa lao, baada ya kubanduliwa mapema katika michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya, msimu huu.