Habari

BBI: Bunge laahirisha vikao vya Jumatano

November 27th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

VIKAO vya bunge vya Jumatano, Novemba 27, 2019, vimeahirishwa kutoa nafasi kwa wabunge kuhuhuria hafla ya kuzinduliwa rasmi kwa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumanne kutoa mwaliko kwa wabunge wote kuhudhuria hafla hiyo ambapo ripoti hiyo itatolewa kwa umma.

“Waheshimiwa Wabunge, kwa misingi ya uteuzi wa jopokazi la maridhiano kupitia ilani kwenye Gazeti Rasmi la Serikali nambari 5154 toleo la Mei 24, 2018, Mheshimiwa Rais ametangaza kuwa kutakuwa na uzinduzi wa Ripoti ya Jokokazi hilo Jumatano, Novemba 27, 2019, katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi kuanzia saa nne asubuhi. Na amewaalika nyote,” Spika Justin Muturi akasema kwenye taarifa aliyosoma katika kikao cha Jumanne alasiri.

Uzinduzi wa ripoti hiyo unajiri saa chache baada ya mwenyekiti wa BBI Yusuf Haji kumkabidhi Rais Kenyatta mnamo Jumanne katika Ikulu ya Nairobi.

Shughuli hiyo ilihudhuriwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto.

Kundi hilo la BBI liliandaa vikao vya kukusanya maoni na mapendekezo kutoka wananchi katika kaunti zote 47.