Habari Mseto

BBI: Gavana Nyoro aongoza wakazi wa Kiambu kutia saini

November 29th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

GAVANA wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro na viongozi wa eneo hilo waliongoza wakazi kutia saini kuidhinisha mswada wa kura ya maamuzi kuhusu ripoti ya BBI.

Viongozi hao walitoa hakikisho kuwa ifikapo Jumatano watakuwa wamelenga saini milioni moja.

Askofu wa Calvary Church mjini Thika Bw David Ngari Gakuyo ambaye pia aliungana na gavana kuongoza mchakato huo alimtaka naibu rais William Ruto kufuata mkondo huo.

“Kulingana na ujumbe wake katika mtandao hivi majuzi, naibu wa rais Dkt Ruto alionyesha kuridhika na ripoti ya BBI iliyofanyiwa mageuzi na iliyozinduliwa siku chache zilizopita,” alisema Askofu Gakuyo.

Aliwahimiza Wakenya wote popote walipo kuipitisha ripoti hiyo kwa sababu italeta manufaa mengi kwao.

Dkt Nyoro alisema ripoti ya BBI italeta manufaa mengi kwa sababu Kaunti ya Kiambu itapata maeneobunge sita zaidi huku akisema Sh600 milioni za fedha za maendeleo (NG-CDF) zitaongezeka zaidi.

Alisema fedha za ugavi kwa kaunti tofauti zitaongezwa hadi asilimia 35 kutoka 15.

“Huu sio wakati wa kuingiza siasa kwa ripoti hiyo bali ni wakati wa kuzingatia manufaa itakayonufaisha mwananchi wa kawaida,” alisema Dkt Nyoro.

Alidai kuwa yeyote anayezidi kupinga ripoti hiyo ni yule hataki kuona manufaa yatakayoletwa kwa mwananchi.

Uzinduzi huo ulifanyika mnamo Ijumaa wiki jana katika maeneo ya Juja na Kiambu, huku wakilenga saini milioni moja ifikapo Jumatano.

Alisihi jamii za Mlima Kenya kuwa mstari wa mbele kuunga mkono ripoti hiyo kwa sababu wao ndio watafaidika pakubwa.

“Tunaelewa hali ya kiuchumi katika eneo hili itaimarika pakubwa na kwa hivyo yeyote anayepinga ripoti hiyo ni adui wa maendeleo,” alisema Dkt Nyoro.

Viongozi wengi kutoka Kiambu wanaotarajia kuwania viti vya kisasa mwaka wa 2022 walikuwa katika mstari wa mbele kuiunga mkono ripoti hiyo ya BBI.

Mawakili kadha kutoka Nairobi na Kiambu, walifika kwa mchakato huo huku wakiwa mstari wa mbele kueleza wakazi wa Kiambu kuwa BBI ni ripoti nzuri na inastahili kuungwa mkono.

Mawakili hao walipitia ripoti hiyo kwa makini huku wakitoa maelezo kwa njia mwafaka ya kueleweka huku wakisema itanufaisha mwananchi wa kawaida.