Siasa

BBI iandikwe kwa hati ya kueleweka na walemavu – Shirika

October 26th, 2020 1 min read

Na Diana Mutheu

SHIRIKA la kutetea haki za walemavu katika Kaunti ya Mombasa limeomba ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), ichapishwe kwa maandishi ya wenye mapungufu ya kuona, ili nao waweze kujisomea kwa urahisi na kutoa maoni yao.

Akizungumza na Taifa Leo, mwanzilishi wa Shirika la Tunaweza, Bi Charity Chahasi alisema iwapo kweli serikali ina nia ya kumjumuisha kila mtu katika mpango huo, basi sharti iweke mikakati ya jinsi watu vipofu na viziwi watakavyoweza kujisomea masuala yote ya BBI.

Hii ni baada ya viongozi wa kisiasa wanaounga mkono BBI kuwaomba na kuwasisitizia Wakenya wajisomee ripoti hiyo wenyewe, ili waweze kutoa maoni ya busara.

“Viongozi hawa wakisema kila mtu ajisomee BBI, wamepanga vipi jinsi vipofu na viziwi watakavyofanya hivyo ilhali ripoti yenyewe haijachapishwa kwa maandishi wanayoweza kuyasoma? Ni vigumu sana. Tunaiomba serikali ichapishe BBI kwa maandishi ya watu walio na ulemavu wa kuona,” akasema Bi Chahasi.

Alisema ni lazima viziwi nao watafutiwe watu ambao wanaweza kuzungumza kwa ishara ili waweze kujua kilichomo katika BBI.

Hivi majuzi, viongozi wa walemavu wakizungumza katika kaunti ya Nairobi walitishia kupinga BBI wakidai kuwa iliwatenga pakubwa.

Pia, baadhi ya walemavu kutoka Mombasa walisema kuwa watapinga BBI, iwapo haitawajumuisha kikamilifu.