BBI ilivyotafuna mabilioni ya mlipa ushuru

BBI ilivyotafuna mabilioni ya mlipa ushuru

Na WANDERI KAMAU

KUHARAMISHWA kwa Mpango wa Marekebisho ya Katiba (BBI) hapo jana ni pigo kubwa kwa mlipa-ushuru, kwa kuwa serikali ilitumia mabilioni ya fedha kuupigia debe.

Inakisiwa kuwa kufikia sasa, karibu Sh10 bilioni zimetumika katika shughuli zote zinazohusiana na mpango huo.Shughuli hizo zinajumuisha marupurupu waliokuwa wakipokea wanachama 14 wa jopokazi maalum la kuendesha mchakato huo, lililoongozwa na aliyekuwa Seneta wa Garissa, marehemu Yusuf Haji.

Jopo hilo liliteuliwa mnamo Januari 2020 na Rais Kenyatta baada ya kufanya mashauriano na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.Wanachama wa jopo hilo walikuwa Askofu Lawi Imathiu, Seneta Maison Leshomo, Bw James Matundura na Bi Rose Moseu.

Wengine ni Seneta Agnes Kavindu (Machakos), Bw Saeed Mwaguni, Askofu Peter Njenga, Askofu Zaccheaus Okoth, Dkt Adams Oloo, Seneta Amos Wako (Busia), Bi Florence Omose, Bw Morompi ole Ronkei na Meja John Seii.

Kando na wanachama hao, jopo pia lilikuwa na makarani ambao walirekodi na kunakili mapendekezo yaliyowasilishwa na makundi mbalimbali kwenye vikao vilivyoandaliwa kote nchini.

Hata hivyo, waliokuwa makatibu wa jopo hilo, wakili Paul Mwangi na Balozi Martin Kimani, walipuuzilia mbali madai hayo, wakisema fedha walizotengewa hazikufikia kiwango hicho.

“Ni kweli tulitengewa fedha ila kiwango kinachotajwa kimetiwa chumvi sana,” akasema Bw Kimani.

Rais Kenyatta pia amekuwa akikosolewa pakubwa kwa kuiagiza Tume ya Kusawazisha Mishahara na Marupurupu (SRC) kugeuza mikopo iliyokuwa imetolewa kwa madiwani kununua magari kuwa ruzuku.

Madiwani walipewa jumla ya Sh4 bilioni kote nchini kama mikopo ya magari.

You can share this post!

Vigogo wa kisiasa kutafuta mbinu mpya kusuka miungano bila...

DOUGLAS MUTUA: Tuwasitiri na tuwapende wakimbizi wa...