BBI inavyofufua ndoto za kisiasa za wanasiasa waliobwagwa 2017 na kuwaweka pazuri kushinda 2022

BBI inavyofufua ndoto za kisiasa za wanasiasa waliobwagwa 2017 na kuwaweka pazuri kushinda 2022

Na CHARLES WASONGA

MCHAKATO wa ukusanyaji wa sahihi za kufanikisha marekebisho ya Katiba kupitia kura ya maamuzi umefufua ndoto za kisiasa za baadhi ya wanasiasa walioteuliwa kushirikisha shughuli hiyo maeneo mbalimbali nchini.

Baadhi ya washirikishi 16 wa kanda walioteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuongoza shughuli hiyo, kila mmoja ana ndoto ya kuwania nyadhifa za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao au wanapania kurejea ulingoni baada ya kubwagwa katika uchaguzi wa 2017.

Bw Dennis Waweru na kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa Junet Mohamed wanaosimamia shughuli hiyo kama wenyeviti wenza wanapania kutumia shughuli hiyo kupiga jeki ndoto zao za kisiasa 2022.

Bw Waweru ambaye alipoteza kiti chake cha Dagoretti Kusini baada ya kubwagwa na John Kiarie katika uchaguzi mkuu wa 2017 anapanga kutumia shughuli ya marekebisho ya Katiba kama ngazi ya kumsaidia kutwaa wadhifa huo kwa matumaini kuwa ataweza kuteuliwa Waziri Serikalini.

Hii ni kwa sababu mswada wa BBI unasema kuwa nusu ya baraza la mawaziri 22 itateuliwa miongoni mwa wabunge, hali ambayo imefanya kiti cha ubunge kuvutia wanasiasa wengi, wakiwemo viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa nchini.

Bw Waweru pia amekuwa akimezea mate kiti cha ugavana wa Nairobi ambao unashikiliwa sasa na Mike Sonko anayezongwa na tishio la kutimuliwa afisini.

Bw Kiarie, maarufu kama KJ anaegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto ambao umekuwa ukipinga mchakato wa marekebisho ya Katiba kabla ya mswada wa BBI kufanyiwa marekebisho machache wiki jana.

Naye Bw Mohamed ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Odinga amekuwa akimezea mate kiti cha ugavana wa Migori ikizingatiwa kuwa Bw Zachary Okoth Obado anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye aliwahi kuhudumu kama Meya wa Migori huenda akabadili nia yake ya kuwania ugavana na badala yake akatetea kiti chake cha ubunge wa Suna Mashariki kama ngazi ya kujiweka pazuri kuteuliwa Waziri.

Katika Kaunti ya Nairobi, Rais Kenyatta na Bw Odinga wamewateua wabunge George Aladwa (Makadara), Simba Arati (Dagoretti Kaskazini) na Mbunge Maalum Maina Kamanda kuongoza shughuli ya ukusanyaji sahihi.

Mbw Aladwa na Arati wana ndoto ya kuwania kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu ujao; Aladwa anataka kuwania Nairobi ilhali Arati anapania kujaribu bahati yake kurithi kiti cha James Ongwae katika kauunti ya Kisii. Bw Ongwae anahudumu muhula wa pili na wa mwisho na hivyo, kikatiba, haruhusiwi kuwania kiti hicho kwa mara ya tatu.

Bw Odinga amefufua nyota ya siasa ya aliyekuwa Mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo kwa kumteua kuwa mshirikishi wa shughuli ya ukusanyaji sahihi katika eneo zima la Nyanza. Bw Midiwo ambaye ni binamuye Bw Odinga, alipoteza kiti chake katika uchaguzi mkuu wa 2017 baada ya kuhudumu kwa miaka 15, alipobwagwa na Bw Elisha Odhiambo katika mchujo wa ODM.

Aligura chama hicho cha Chungwa na kutetea kiti chake kama mgombeaji huru lakini akashindwa tena na Bw Odhiambo katika uchaguzi mkuu.

Mbunge wa Borabu Benjamin Momanyi ameteuliwa kuwa mshirikishi wa shughuli ya ukusanyaji sahihi katika Kaunti ya Nyamira. Mwanasiasa huyu, ambaye ni mwandani wa karibu wa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, ambaye pia anatoka Nyamira, amekuwa akimezea mate kiti cha ugavana wa kaunti. Hii ni kwa sababu Gavana John Nyagarama anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho.

Bw Momanyi ambaye pia ni Kamishna katika Tume ya Huduma za Bunge (PSC) Anapania kutumia shughuli hiyo ya BBI kujinadi kwa wananchi katika jitihada za kufanikisha ndoto yake.

Katika kaunti ya Kisii, Bw Patrick Lumumba ambaye aliwania kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu wa 2017 ndiye aliteuliwa kuwa mshirikishi wa ukusanyaji sahihi. Anatarajiwa kutumia nafasi hii kuimarisha ushawishi wake kwa wananchi kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Aliyekuwa Seneta wa Embu Lenny Kivuti ambaye aliteuliwa mshirikisha wa ukusanyaji wa sahihi za BBI alisema kuwa atahakikisha kuwa shughuli hiyo imefanikiwa ipasavyo.

Bw Kivuti, ambaye alibwagwa na Gavana Martin Nyaga Wambora katika uchaguzi mkuu uliopita anatarajiwa kujaribu bahati yake kwa mara nyingine kwa kuwania kiti hicho.

“Shughuli hii isichukuliwe kama jukwaa la kuwajenga watu fulani kisiasa bali kama mpango wa kufanikisha marekebisho ya Katiba kwa manufaa ya Wakenya wote,” akasema Bw Kivuti mnamo Jumatatu, Novemba 30, 2020.

Katika eneo la Kati mwa Kenya ushirikishi wa shughuli hiyo unaongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Mathira Peter Weru. Mwanasiasa huyo alibwagwa na mbunge wa sasa Rigathi Gachagua ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.

Katika eneo zima la South Rift wajibu huo umetwikwa aliyekuwa Waziri Paul Sang’ ambaye aliwania kiti cha useneta wa Kericho na akashindwa na Aaron Cheruiyot, mwandani wa Dkt Ruto.

Bw Sang’ ambaye ni mshirika wa Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi anatarajiwa kutumia nafasi hiyo kuimarisha nafasi yake ya kuwania kiti cha ugavana wa Kericho ambacho anakimezea mate. Gavana Paul Chepkwony anahudumu kipindi chake cha pili na cha mwisho na hivyo hatatetea kiti hicho 2022.

Magavana wote wametwikwa jukumu la kusimamia shughuli ya ukusanyaji sahihi katika kaunti na maeneo wanakotoka ambapo Gavana Wycliffe Oparanya anasimamia shughuli hiyo katika eneo zima la Magharibi.

You can share this post!

Kirui na Rono waanika maazimio yao kwenye Valencia Marathon

Polisi wamtoa Sonko machozi mkutanoni