BBI: Karua adai Uhuru alinyakua mamlaka ya raia

BBI: Karua adai Uhuru alinyakua mamlaka ya raia

Na RICHARD MUNGUTI

KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya, Bi Martha Karua, na wakili mashuhuri John Khaminwa, Ijumaa waliongoza mawakili 10 kumkosoa Rais Uhuru Kenyatta, kwa kuasisi mchakato wa kubadilisha Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano ­(BBI).

Bi Karua na Bw Khaminwa waliambia Mahakama ya Rufaa kwamba Rais Kenyatta alinyakua mamlaka ya Wakenya alipoasisi mchakato huo.

Hivyo, mawakili hao waliomba Mahakama ya Rufaa isivuruge uamuzi wa majaji watano wa Mahakama Kuu, walioamua kwamba mwananchi wa kawaida ndiye mwenye mamlaka ya kuanzisha marekebisho ya Katiba wala sio maafisa wakuu serikalini.

Huku wakiwaomba majaji wa rufaa kukubali uamuzi wa wenzao watano wa Mahakama Kuu – uliosimamisha mchakato huo wa BBI – Dkt Khaminwa na Bi Karua walisema Rais aliteka haki ya mwananchi wa kawaida kwa kuasisi marekebisho hayo kupitia BBI.

Dkt Khaminwa alisema rufaa aliyowasilisha Rais Kenyatta yapasa kutupiliwa mbali; kwa sababu huwa hatii maagizo ya mahakama, na hukiuka mara kwa mara Katiba.

Alitoa mfano wa Rais kukataa kuwaapisha majaji 41 walioidhinishwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

“Waandalizi wa Katiba ambayo ndiyo sheria kuu ya nchi hawakuruhusu viongozi waliochaguliwa kuasisi marekebisho ya katiba,” alisema.

Bi Karua aliomba mahakama kutumia uwezo iliyopewa na Katiba kuwaadhibu wanasiasa wanaotaka kutumia ushawishi wao kukiuka sheria hiyo kuu yaa nchi.

Kinara huyo wa Narc Kenya aliongeza kwamba Mahakama ya Rufaa ina nguvu sawa na zile za viongozi wa Serikali ya Kitaifa, na kwamba mihimili yote ya serikali inapata nguvu kutoka kwa wananchi.

“Nguvu za mahakama hii sio duni kuliko za Serikali Kuu; mihimili yote ya serikali hutoa nguvu zao kwa raia, na mahakama hii ina uamuzi wa mwisho wa kutafsiri Katiba,” alikariri Karua.

Alihoji kuwa wanasiasa wakuu nchini wanataka kubadilisha Katiba kwa nia ya kuendelea kuwa mamlakani.

“Katiba huwekwa ili kuzima matumizi mabaya ya mamlaka na inaoenekana hii haieleweki kwa viongozi wa serikali ya Kenya,” akasema.

Bi Karua aliomba korti hiyo ya rufaa kuagiza maafisa wa serikali ambao wamekuwa wakitumia pesa za umma katika mchakato huo haramu, wazilipe.

Zaidi, anataka mahakama kutupilia mbali rufaa ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliozima BBI.

“Ni kupitia uamuzi wa mahakama hii, bila woga au mapendeleo, ambapo nchi hii itaafikia mageuzi yaliyotazamiwa wakati Katiba ya 2010 ilipitishwa,” aliongeza.

Rais wa Mahakama ya Rufaa, Daniel Musinga, majaji Roselyn Nambuye, Hannah Okwengu, Patrick Kiage, Kairu Gatembu, Fatuma Sichale na Francis Tuiyot wanasikiliza rufaa iliyowasilishwa na Rais Kenyatta, Ofisi ya BBI, Mwanasheria Mkuu, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Mawakili Dudley Ochiel, Ian Mathenge, Edga Busiega , Christian Adole, Evans Ogada, Elisha Ongoya na Muthoni Nyaguto waliomba majaji hao wasihofu bali watupe nje rufaa hiyo.

Bw Adole aliomba mahakama iamuru Rais Kenyatta awarudishie umma pesa zilizotumiwa na kamati ya BBI, aliyoiteua kuzunguka nchini kupokea maoni ya wananchi.

You can share this post!

Italia kukutana na Uhispania kwenye nusu-fainali za Euro...

Mourinho atua Italia kuanza kazi ya ukocha kambini mwa AS...