BBI: Kibarua kwa wabunge kushawishi wafuasi

BBI: Kibarua kwa wabunge kushawishi wafuasi

Na GEORGE ODIWUOR

VIONGOZI kutoka eneo la Nyanza wanaounga mswada wa mabadiliko ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) wanakabiliwa na kibarua kuelezea wapiga kura sababu eneo hili litapata maeneo bunge machache ikiwa mswada huo utapita katika kura ya maamuzi.

Viongozi hao wanatarajiwa kuandaa msururu wa mikutano ya kampeni sio tu kuvumisha mswada huo lakini pia kuelezea wakazi kwanini maeneo mengine yalipata maeneo bunge mengi ilhali Nyanza ilipata maeneo bunge manne pekee.

Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma alisema wale wanaopinga mabadiliko hayo ya Katiba huenda wakatumia mfumo wa ugavi wa maeneo bunge 70 yaliyopendekezwa katika mswada huo kuendesha kampeni ya kuupinga.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga, ambaye ana ufuasi mkubwa Nyanza, amekuwa akiunga mkono Mswada huo wa BBI, licha ya kwamba eneo hilo lipataka maeneo bunge manne pekee.

Ngome ya kisiasa ya Naibu Rais William Ruto, Rift Valley, ndio itafaidi pakubwa kwa kupata maeneo bunge 23 mapya, ikifuatwa na Nairobi ambayo imetengewa maeneo bunge 12, eneo la Kati mwa Kenya (11) huku Pwani ikipata maeneo 10 mapya.

Eneo la Magharibi litatunukiwa maeneo bunge matano, Ukambani (4) na Kaskazini Mashariki litapata eneo moja pekee zaidi, endapo mswada wa BBI utapitishwa.

Bw Kaluma alielezea hofu kwamba, baadhi ya wakazi wa kaunti za Homa Bay na Migori, ambazo hazitapokea maeneo bunge zaidi, huenda wakashawishiwa kupinga mswada huo katika kura ya maamuzi.

“Kama viongozi kutoka Nyanza, na wabunge ambao ni mawakili, tumeamua kuwahamasisha watu wetu kuhusu jinsi maeneo mapya yalifikiwa na kwa nini baadhi ya kaunti zitafaidi zaidi kuliko zingine.”

Haya yanajiri baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha mswada huo wa BBI wakati wa kikao cha Alhamisi wiki jana kilichoendelea hadi saa sita kasoro dakika 10 za usiku. Wiki hii maseneta wanatarajiwa kukamilisha mjadala kuhusu mswada huo na kisha kupiga kura ya kuupitisha au kuukataa kabla ya mswada huo kuwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta.

You can share this post!

Joho, Ruto waua ndoto ya chama cha Wapwani

Changamoto tele wanafunzi wakirejea shuleni