Habari

BBI: Kimya chao chazua hofu

November 21st, 2020 2 min read

BENSON MATHEKA Na CECIL ODONGO

KUAHIRISHWA ghafla kwa hafla ya ukusunyaji wa saini milioni moja za kuunga ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), kumezua hofu kuhusu hatima ya mchakato huo huku Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wakisalia kimya.

Ingawa taarifa kutoka kwa afisi inayoshughulikia mchakato huo ilisema kwamba hafla hiyo iliahirishwa kwa kuwa mswada haukuwa umechapishwa, hakukuwa na kauli rasmi kutoka kwa vinara hao.

Kabla ya wenyekiti wenza wa mchakato huo, Junet Mohammed na Dennis Waweru kutangaza kuwa hafla hiyo haingefanyika Alhamisi, Bw Odinga alikuwa akizungumzia BBI kila siku huku akishawishi makundi yanayoipinga kuiunga.

Alikuwa akisisitiza kuwa mchakato huo haungesitishwa ili kuwapa nafasi wanaolalamika na kimya chake baada ya hafla kuahirishwa kimefanya wafuasi wake kuwa na wasiwasi.

Ripoti zilisema kwamba Bw Odinga aliondoka nchini Alhamisi usiku kwa ziara ambayo haikutangazwa.

Mnamo Alhamisi, Rais Kenyatta alizuru kambi ya kikosi cha kulinda mipaka eneo la Kanyonyoo kaunti ya Kitui ambapo alizungumzia masuala ya usalama.

Ijumaa, aliendelea na shughuli zake za kawaida bila tamko la kuashiria hali ya mchakato huo.

Wandani wa viongozi hao waliokuwa wakipigia debe pia wameonekana kutulia.

Huku wafuasi wa vinara hao wakiwa na maswali, wanasiasa wanaoegemea upande wa Naibu Rais Dkt William Ruto walisifia hatua hiyo wakisema sasa kuna nafasi ya maoni yao na wanaolalamika kuzingatiwa kabla ya kura ya maamuzi.

Shughuli hiyo iliyofaa kufanyika Alhamisi iliahirishwa dakika za mwisho baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuandaa mkutano na Dkt Ruto.

Kufuatia kimya cha wawili hao, maswali yameibuka kuhusu nini hasa kilichosababisha hafla hiyo kuahirishwa.

Bw Waweru na Bw Mohammed wanasema mswada wa BBI haukuwa umechapishwa ndio maana hafla hiyo ikaahirishwa. Hata hivyo, duru kutoka afisi ya mchapishaji wa serikali ilikanusha madai hayo.

Pia inadaiwa uzinduzi huo uliahirishwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya maambukizi ya virusi vya corona, ikisemekana serikali inataka kumakinikia kupambana na janga hilo kwanza.

Kulingana na seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, kuahirishwa kwa uzinduzi wa ukusanyaji wa saini ulichangiwa na juhudi za Dkt Ruto za kutaka maswala yote tata yasuluhishwe na maoni ya makundi mbalimbali yajumuishwe kwenye BBI.

Bw Murkomen ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto pia alishikilia msimamo kuwa hakuna haja ya Kenya kuandaa kura ya maamuzi ya kuwagawanya wananchi ilhali vilio vya makundi mbalimbali vinaweza kujumuishwa kupitia muafaka kuhusu BBI.

Hata hivyo, baadhi ya wandani wa Bw Odinga na Rais Kenyatta wanadai Dkt Ruto hakumshawishi kiongozi wa nchi kuahirishwa hafla hiyo.

“Kuahirishwa kwa hafla hiyo kulichangiwa na kucheleweshwa kwa kuchapishwa kwa ripoti ya BBI,” akasema mbunge wa Nyeri mjini Ngunjiri Wambugu.

Katibu wa kamati ya BBI Paul Mwangi naye kwenye akaunti yake ya Twitter alisema mswada huo upo tayari lakini hakubainisha iwapo kauli hiyo ilimaanisha mswada tayari umechapishwa.

“Mswada upo tayari na tunatarajia kupata tarehe mpya ya uzinduzi wa saini,” akasema.