BBI kuangushwa katika kura ya maamuzi – Utafiti

BBI kuangushwa katika kura ya maamuzi – Utafiti

Na CHARLES WASONGA

UTAFITI wa hivi punde unaonyesha kuwa Wakenya watakataa mswada wa mageuzi ya Katiba kupitia mchakato wa BBI endapo kura ya maamuzi ingefanywa hii leo.

Kulingana na matokeo ya utafiti huo yaliyoendeshwa na Shirika la TIFA asilimia 32 ya wapigakura watapiga kura ya LA huku asilimia 29 wakipiga kura ya NDIO.

Utafiti huo ambao matokeo yake yalitolewa Ijumaa, Januari 8, 2021, asilimia 26 ya wapigakura hawatashiriki katika kura hiyo ya maamuzi huku asilimia 16 hawana uhakika ikiwa watashiriki shughuli hiyo au la kwa sababu hawana habari kuhusu yaliyomo kwenye ripoti ya BBI.

Wengine wao pia wanaamini kuwa kutakuwa na udanganyifu katika kura hiyo ya maamuzi hivi kwamba matokeo hayataakisi msimamo wa wapigakura.

Asilimia 32 ya wale ambao watapiga kura ya LA watafanya hivyo kwa sababu hawana habari kuhusu mchakato huo, asilimia 32 watapiga kura kwa sababu wanahisi kuwa suala hilo halifai kupewa kipaumbele wakati huu, asilimia 20 watakataa BBI kwa sababu itaongeza joto la kisiasa nchini huku asilimia tisa wakiikataa kwa sababu wanahisi imeongeza mamlaka katika afisi ya rais.

Kwa upande mwingine asilimia 26 ya wale watakaopiga kura ya NDIO watafanya hivyo kwa sababu ya pendekezo la kuongezwa kwa fedha kwa kaunti hadi asilimia 35, asilimia 19 wataunga mkono kwa sababu mswada huo wa BBI unabuni nyadhifa za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili, asilimia 15 watapiga kura ya NDIO kwa sababu BBI inafaidi vijana huku asilimia 5 wakipiga kura jinsi hiyo kwa sababu BBI inabuni wadhifa wa Kiongozi Rasmi wa Upinzani.

Na asilimia 40 ya wapigakura watakaounga mkono mswada wa BBI hawakutoa sababu zitakazochangia wao kupiga kura kwa njia hiyo.

“Hii ina maana kuwa wale wanaopigia debe BBI na wale wanaoipinga wangali na kibarua kikubwa kuwashawishi Wakenya kuunga mkono misimamo yao,” ikasema ripoti hiyo ya TIFA.

Matokeo ya utafiti huo yametolewa siku nne baada ya barua ambayo kiranja wa wengi katika Seneti Irungu Kang’ata alimwandikia Rais Uhuru Kenyatta ikisema kwamba wakazi wengi wa Mlima Kenya hawataki BBI kuibua cheche katika ulingo wa kisiasa.

Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a alisema kuwa alimwandikia Rais Kenyatta baada ya kufanya utafiti wake binafsi uliobaini kuwa ni watu wawili pekee kati ya watu sita eneo hilo wanaunga mkono BBI.

Eneo la Mlima Kenya ni ngome ya kisiasa ya Rais Kenyatta ambaye pamoja na Kiongozi wa ODM Raila Odinga ndio waasisi wa mchakato wa BBI.

You can share this post!

South C Ladies: Soko inavyowasisimua mabinti wa mitaani

Gor Mahia kujua mpinzani wao kwenye mchujo wa Kombe la...