Habari MsetoSiasa

BBI: Lengo ni kuzuia vita kila baada ya uchaguzi

November 28th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

CHAGUZI zenye kuleta migawanyiko ni mojawapo ya changamoto tisa ambazo zilitambuliwa katika mwafaka uliowekwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, kama zinazosababisha machafuko kila baada ya miaka mitano.

Kulingana na ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) iliyozinduliwa jana, hali hiyo husababishwa na ushindani mkali wa wadhifa wa urais, cheo chenye hadhi ya juu zaidi katika siasa za Kenya.

Na, kulingana na ripoti hiyo, chaguzi zenye migawanyiko huchochewa zaidi na siasa za kikabila ambazo zimedumu nchini tangu mwaka wa 1992, baada ya kurejelewa kwa mfumo wa utawala wa vyama vingi nchini.

Vile vile, ripoti hiyo inasema chaguzi zenye migawanyiko husababishwa na ukosefu wa uongozi ambao unawahusisha kwa wote katika kitengo cha utawala wa nchi.

“Kwa hivyo ili kuzuia kurejelewa kwa chaguzi za kuleta migawanyiko, jopokazi hili limependekeza kupanuliwa kwa kitengo cha utawala kwa kupendekeza kuwa kutakuwa na Rais mwenye mamlaka makuu ambaye atakuwa Kiongozi wa Nchini na Serikali.

“Rais naye atateua Waziri Mkuu ambaye atakuwa akiendesha shughuli za kila siku na sera za nchi,” ripoti hiyo ikasema.

Ripoti hiyo inasema kuwa mfumo huo ndio huendelezwa katika mataifa ya ng’ambo yaliyokumbatia utawala wa kidemokrasia.

“Na tofauti na hali ilivyo katika mataifa ya ng’ambo, chaguzi zetu nchini Kenya zimehusishwa na dhana kuwa mshindi ndiye hutwaa mamalaka yote. Hii ndio maana tumeshuhudia chaguzi zenye migawanyiko kila baada ya miaka mitano, mwenendo ambao sasa tunataka kuukomesha,” ikasema ripoti hiyo.

Hii ndio maana akiongea jana katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, Rais Kenyatta alikariri kuwa lengo la BBI ni kuhakikisha mshindi katika uchaguzi anachukuliwa kama kiongozi wa “walioshinda na walioshindwa”.

“Tunataka hali ambapo Rais atakayeshinda atakubalika na wote, wakiwemo wale ambao mgombeaji wao alishindwa. Tunataka mbunge au diwani atakayetangazwa mshindi awe anakubalika na wale wote walioshindwa, pamoja na wafuasi wao,” akasema.

Rais Kenyatta alitoa kumbukumbu ya hali ya machafuko yaliyotokea baada ya chaguzi za miaka ya 2007, 2013 na 20017 wakati ambapo matokea ya urais yalibishaniwa.

“Nilisalimiana na ndugu yangu Raila Odinga ili kukomesha hali kama hizi katika uchaguzi mkuu ujao wa 2022 na chaguzi nyinginezo zijazo,” akasema.

Wakati huo huo, ripoti ya BBI pia imependekeza kuwepo kwa ujumuishaji katika nyanja za uongozi, kisiasa na kiuchumi ili kuondoa dhana ya kutengwa kwa maeneo fulani ya nchi.

Vile vile, wanachama wa jopo hilo wanasema wananchi waliotoa maoni katika vikao vyake walipendekeza kuwa rasilimali ya nchi igawanywe kwa misingi ya wingi wa watu.

“Wananchi walichukizwa na hali ambapo uwezo wa kura zao nyingi hauchukuliwi kwa uzito. Wale walio wengi wameendelea kulalamika kwamba kura zao hazipewi uzito stahiki,” ripoti hiyo inaeleza.

Suala kuu katika dhana hii ya ujumuishaji ni kwamba sharti ionekane ikitekelezwa haswa katika uteuzi wa maafisa katika Utumishi wa Umma.

“Uteuzi huo sharti uonekane kuzingatia usawa wa kikabila, kidini, kimaeneo na kitamaduni. Kimsingi, sura ya kitaifa inapasa kuonekana katika uteuzi wa maafisa wakuu katika utumishi wa umma. Na uteuzi huo haupasi kuingizwa ufisadi.

Ripoti hii ya BBI pia inalenga kuhakikisha kuwa serikali za kaunti zinazingatia usawa katika uajiri wa watumishi wa umma na teuzi za watu katika nyadhifa za juu.