BBI: LSK yadai ni rais alianzisha mageuzi

BBI: LSK yadai ni rais alianzisha mageuzi

Na RICHARD MUNGUTI

CHAMA cha Wanasheria nchini (LSK) na kile cha Thirdway Alliance, Alhamisi vilipinga madai kuwa walioanzisha mpango wa kubadili katiba kupitia BBi ni Mbunge Junet Mohamed na Dennis Waweru.

Pande hizo mbili zilipopata fursa ya kujibu madai ya mawakili wa Rais Uhuru Kenyatta, Raila Odinga na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), walisisitiza kuwa shughuli hiyo ilizinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Kufanya hivyo ni kinyume cha Katiba, kwa kuwa yafaa mageuzi yaanzishwe na raia asiye na mamlaka yoyote.

“Rais hana mamlaka kikatiba kuzindua mageuzi ya katiba. Hawezi kulisukuma bunge lipitishe hoja ya mageuzi ya katiba. Kamwe hana mamlaka kama hayo,” alisema Rais wa LSK, Bw Nelson Havi.

Alidai Rais Kenyatta alizindua mageuzi hayo alipopokea ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) kutoka kwa kamati ya kitaifa iliyoongozwa na marehemu Yusuf Haji.

Wakili Elias Mutuma kwa niaba ya Thirdway alisema ni wananchi wanaopaswa kuzindua marekebisho ya katiba na wala sio Rais aliye na mamlaka makuu.

“Ni handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga iliyobuni BBI ambayo ilipendekeza mageuzi ya katiba. Katiba imetoa utaratibu wa kufanyiwa mageuzi yakizinduliwa na wananchi na wala sio wakuu serikalini,” akasema.

Mawakili hao wanawataka majaji saba wanaosikiliza rufaa hiyo, wadumishe uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu suala hilo.

Majaji saba wakiongozwa na Rais wa Mahakama ya Rufaa Daniel Musinga ni Roselyn Nambuye, Hannah Okwengu, Patrick Kiage, Kairu Gatembu, Fatuma Sichale na Francis Tuiyot.

You can share this post!

Ruto aahidi wapiga kura bondeni uhuru wa kuamua

Besigye achemkia Museveni kupanda kwa visa vya corona