BBI: Maadili kuwa funzo la lazima kuanzia nasari hadi chuoni

BBI: Maadili kuwa funzo la lazima kuanzia nasari hadi chuoni

Na WANDERI KAMAU

MOJAWAPO ya mapendekezo ya ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) ni kufundishwa kwa maadili kama somo la lazima shuleni.

Ripoti hiyo inapendekeza somo hilo lifunzwe kutoka nasari hadi chuo kikuu. Inapendekeza suala la utaifa lijumuishwe katika somo hilo kama sehemu ya tamaduni za jamii mbalimbali, hasa hatua ambazo mtu anafuata kuelekea utu uzima.

Inaeleza kuwa utekelezaji wa suala la maadili unapaswa kuwianishwa na Sura ya Sita ya Katiba kuhusu Maadili na Uwajibikaji.

Inaeleza kuwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inapaswa kulenga zaidi kwenye juhudi za kuzima makosa yoyote yanayohusiana na uhalifu wa kiuchumi.

Ripoti inapendekeza kuwa suala la maadili linapaswa kuelekezwa kwa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC).

Na mbali na kuwa itakuwa ikisimamia masuala ya maadili, inapendekeza NCIC kubadilishwa jina kuwa Tume ya Maadili.

Tume hiyo itakuwa chini ya Afisi ya Rais.Pendekezo lingine la ripoti ni kuwa, serikali inapaswa kuchukua hatua zitakazoimarisha utambulisho wa Kenya kwa uwiano wa tamaduni za Kiafrika.

Hili linalenga kuhakikisha kuwa Wakenya wanaridhika weusi wao.Inaeleza kuwa serikali inapaswa kuipa nguvu Wizara ya Utamaduni na Turathi za kitaifa, kinyume na sasa ambapo huwa haichukuliwi kwa uzito.

Ripoti hiyo pia inapendekeza serikali inapaswa kuondoa Sikukuu ya Kufungua Zawadi mnamo Desemba 26 kuwa Siku ya Kitaifa ya Utamaduni kwa Wakenya kusherehekea tamaduni zao na kujifunza kuhusu tamaduni mpya.

Hili pia linaweza kufanywa katika Januari 1, kila mwaka.Kando na hayo, inapendekeza Rais Uhuru Kenyatta ashinikize mikakati maalum ya kuandika rasmi Historia Maalum ya Kenya.

Uandishi huo utaongozwa na Afisi Maalum ya Mwanahistoria katika Makavazi ya Kitaifa.

You can share this post!

BBI: Wakenya kupata fursa kukagua mali ya rais na wakuu...

BBI: Wadhifa wa ugavana Nairobi hatarini

adminleo