BBI: Magari kwa madiwani, wilbaro kwa vijana

BBI: Magari kwa madiwani, wilbaro kwa vijana

Na BENSON MATHEKA

VUTA nikuvute kuhusu mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), imefanya wanaounga na kupinga zoezi hilo kutafuta mbinu za kutimiza malengo yao.

Kwa wiki chache zilizopita sasa, madiwani wameanza kuvuna kwa vile wana umuhimu mkubwa katika mpango huo mzima.

Madiwani walifanikiwa kuwashinikiza Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga watumie ushawishi wao ili watengewe ruzuku ya kununua magari ya kifahari yatakayogharimu takriban Sh2 milioni kwa kila diwani.

Na kwa upande mwingine, Rais Kenyatta sasa ameahidi vijana kwamba, serikali itarejesha mpango wa Kazi Mitaani, hatua inayoonekana kuwarai waunge mchakato huo.

Nao wapinzani wa BBI, wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto, wamekuwa wakifadhili wananchi wenye biashara ndogo ili kuwavutia upande wao.

Tayari madiwani wa mabunge 11 ya kaunti yamepitisha mswada huo. Rais Kenyatta aliwapa ahadi hiyo alipokutana na madiwani wa kaunti za eneo la Mlima Kenya katika ikulu ndogo ya Sagana mapema mwezi huu.

Tume ya Mishahara (SRC) iliidhinisha ruzuku hiyo licha ya malalamishi kutoka kwa Wakenya waliosema ilinuiwa kuwahonga madiwani ili wapitishe mswada wa BBI.

Jana, Rais Kenyatta aliwaambia vijana kwamba, serikali itaweka mipango ya kuongezea muda mpango wa kazi mitaani ambao ulipangiwa kusitishwa mwishoni mwa mwezi huu.

Mpango huo uliogharimu zaidi ya Sh10 bilioni ulianzishwa mwaka jana kusaidia vijana wa mitaa ya mabanda mijini kujikimu kimaisha kufuatia athari za janga la corona. Jumla ya vijana 250,000 walishirikishwa kwa kazi za kudumisha usafi katika mitaa wanamoishi na maeneo mengine mijini wakitumia vifaa kama wilibaro, vifagio na majembe.

Akizungumza katika mtaa wa mabanda wa Soweto, Kayole jijini Nairobi alipopigia debe mswada wa BBI baada ya kufungua hospitali mpya iliyojengwa na Idara ya Huduma ya Nairobi (NMS), Rais Kenyatta alisema serikali itafufua mpango huo ili vijana waendelee kujipatia riziki.

“Nilipokuwa Uthiru na Kiamaiko kufungua mradi kama huu, vijana waliniambia wanataka mpango wa kazi mitaani urudi. Tutaongea kama serikali, tuweke mipango ili vijana waendelee kupata mkate wao wa kila siku,” alisema huku akishangiliwa na vijana jinsi aliposhangiliwa na madiwani baada ya kuwaahidi pesa za kununua magari.

Ahadi hii inachukuliwa kuwa ya kuwarai vijana ili waweze kuunga mswada wa BBI ikizingatiwa kwamba, Rais Kenyatta na viongozi wanaounga mchakato huo wamekuwa wakikosoa Dkt Ruto kwa kuwapa vijana wilibaro ili washiriki kazi za mikono mitaani.

Kupitia kampeni yake ya hasla, Naibu Rais amekuwa akiahidi watu wa mapato ya chini kwamba, atabadilisha uchumi kuanzia mashinani kwa kuwawezesha wajiimarishe kiuchumi akishinda urais.

Rais Kenyatta aliwaambia wakazi wa Nairobi kuunga mkono mswada wa BBI akisema marekebisho ya katiba yaliyopendekezwa yananuia kuwafaidi.

“BBI haitanifaidi kwa sababu sitakuwa rais. Msidanganywe na watu kwamba mpango huu ni mbaya kwa sababu sio kweli,” alisema Rais Kenyatta.

Alionya Wakenya wasikubali kugawanywa kwa mirengo mbalimbali akisema wanaotaka kufanya hivyo wanataka kuzua vita na umwagikaji damu nchini.

Alisema tangu handisheki yake na Bw Odinga, Wakenya wamekuwa na amani.

“Wakenya wanaishi kwa amani, wanatembea pamoja, wanaishi kama ndugu, nilifanya ubaya gani (kushirikiana na Raila) jameni?

You can share this post!

Utata wa uteuzi wa Mwende Mwinzi waendelea kutokota

Kufungwa kwa hoteli ya kihistoria pigo kwa maskauti