BBI: Majaji watano walivyozima midundo ya Reggae

BBI: Majaji watano walivyozima midundo ya Reggae

Na SAMMY WAWERU

MAHAKAMA Kuu  Alhamisi jioni ilizima mchakato wa Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ikiutaja kuwa haramu, batili na tupu hatua ambayo imetafsiriwa kuwa pigo kubwa kwa jitihada za Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga kufanyia Katiba marekebisho.

Korti kupitia uamuzi wake, ilihoji Rais Kenyatta alitumia vibaya mamlaka yake na kuenda kinyume cha sheria kukarabati Katiba.

Jopo la majaji watano wa mahakama kuu pia lilisema Rais alienda kinyume na kipengele cha sita cha Katiba, kinachoeleza kuhusu uongozi na uadilifu (wa Rais), kwa kujaribu kubadilisha Katiba kupitia mswada haramu wa BBI.

Uamuzi huo uliotolewa saa tatu na nusu usiku, uliorodhesha makosa kadhaa aliyotekeleza Rais Kenyatta katika jitihada zake kufanyia Katiba marekebisho. Aidha, mahakama kuu ilisema mengine yalifanywa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Korti ilitoa amri ya kudumu kwa IEBC kutoandaa zoezi la kura ya maoni, hadi pale itakapotayarisha rejista halali ya wapiga kura na hamasisho kuhusu haja ya Katiba kurekebishwa kufanywa.

BBI iliasisiwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga, baada ya kutangaza kuzika tofauti zao za kisiasa mnamo Machi 2018, kupitia salamu za maridhiano maarufu kama Handisheki.

Masuala yaliyoibuliwa kupitia ripoti ya uamuzi wa Alhamisi wa korti, ulitolewa kiasi kuwa hakutakuwa na ukataji rufaa wowote.

Baadhi ya wanaharakati na mashirika yalielekea mahakamani kupinga uhalisia wa BBI. Viongozi kadha wa upinzani nchini walikuwa wanaunga mkono BBI.

Handisheki kati ya Rais Kenyatta na Odinga, ilichangia mrengo tawala wa Jubilee kugawanyika, vuguvugu moja, Kieleweke, likiegemea upande wa Rais na lingine, Tangatanga upande wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto.

“Kuna Mungu aliye juu mbinguni anayependa Kenya bila kipimo. Jina la Mungu liinuliwe,” Dkt Ruto na ambaye amekuwa mkosoaji wa BBI akachapisha katika ukurasa wake wa Twitter, baada ya uamuzi kuharamisha BBI kutolewa.

Azma ya Rais Kenyatta kubadilisha Katiba kupitia BBI, ilichangia baadhi ya viongozi na wanasiasa Jubilee kufurushwa kutoka nyadhifa zao bungeni na pia katika kamati mbalimbali, kama vile mbunge wa Garissa Mjini, Bw Aden Duale na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen kutokana na msimamo wao mkali, kukosoa mswada huo.

Mahakama kuu kwenye uamuzi wake uliosomwa kwa muda wa saa tano na nusu mfululizo, ilisema kamati ya kiufundi ya wanachama 14 walioteuliwa kukusanya maoni ya Wakenya na kuandaa BBI, ilikuwa haramu na ambayo haikutambulika kisheria.

Kamati hiyo iliongozwa na aliyekuwa seneta wa Garissa, Bw Yusuf Hajii.

Uamuzi huo wa aya 743, ulikuwa mrefu kiasi kuwa majaji waliusoma kila mmoja kwa awamu yake.

Jopo la majaji hao watano, na lililoongozwa na Prof Joel Ngugi, lilisema Rais Kenyatta alifanya kosa kubwa kwa kujaribu kurekebisha Katiba kupitia mswada maarufu, na ambao haukufuata sheria.

Ilieleza, badala yake Rais angetumia bunge la kitaifa kupitia Mwanasheria Mkuu, kukarabati Katiba.

Aidha, korti ilisema marekebisho ya Katiba hayana shotikati ila kutumia asasi ya bunge na mswada maarufu uliofuata sheria.

Mahakama kuu ilisema BBI ilikuwa “mpango” wa Rais, uliochukuliwa kama njia halali kubadilisha Katiba, na kuruhusu sheria kubadilishwa kupitia mkondo huo ingeonekana kama kumpa Rais mwanya wa urefarii kuafikia mipango yake.

“Haiwezi ikawa Rais ndiye mwasisi au mwanzilishi wa Katiba kufanyiwa marekebisho,” mahakama hiyo ikasema, ikiongeza kuwa BBI iliongozwa na tamaa za ubinafsi.

Majaji walisema Rais alivuka mipaka ya mamlaka yake, kupendekeza Katiba ikarabatiwe, ilhali sheria imeweka wazi majukumu yake kama kiongozi wa nchi.

Kwa waliodhania Rais Kenyatta alilenga kuleta umoja wa taifa kupitia pointi tisa zilizoorodheshwa katika mswada huo, korti ilisema dai hilo limesalitiwa na ukweli kuwa jopokazi la BBI liliundwa na Rais mwenyewe na lilikuwa likiripoti kwake.

“Ukweli ni kwamba BBI ilikuwa mpango wa Rais na uliokiuka kipengele cha 257 cha Katiba. Jopokazi lililoundwa lilikuwa haramu tangia mwanzo,” majaji wakasema.

Jopo la majaji hao lilizima tetesi za waliolinganisha BBI na jitihada za Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki kubadilisha Katiba 2005 na 2010, chini ya utawala wake.

Majaji walisema Bw Kibaki alifanya mabadiliko kwa kufuatia sheria za Katiba ya awali, iliyoasisiwa wakati wa utawala wa Mbeberu. Katiba ya sasa, ilizinduliwa 2010 na kuanza kutumika 2013.

Chini ya Katiba ya sasa, majaji hao walisema imeweka wazi kuhusu marekebisho, ila kupitia mswada maarufu na Rais aliye madarakani, afisi ya Rais au asasi ya serikali, hazijaorodheshwa.

Walisema kisheria mapendekezo ya marekebisho ya Katiba yanapaswa kuanzishwa na raia binafsi au kundi la raia binafsi, lakini si asasi ya serikali.

Wanaounga mkono BBI waliambia mahakama kuwa Rais alitumia haki yake Kikatiba, kufanya ukarabati. Majaji hata hivyo walisema Rais alishindwa kulinda Katiba, na kukiuka kifungu kinachoeleza kuhusu uongozi wake na uadilifu.

“Huku jitihada zake kuunganisha taifa na kuleta umoja zikipigiwa upatu, hawezi akaanzisha mpango kurekebisha Katiba. Hatua hiyo haipo chini ya majukumu yake kama kiongozi wa nchi,” korti ikasisitiza.

Majaji walisema kwa sababu mpango huo ulikuwa haramu tangia awali, yote yaliyolengwa kuafikiwa hayataleta mtafaruku wowote kisheria, baada ya kuuharamisha.

Mahakama kuu pia ilisema Rais Uhuru Kenyatta (kama rais aliye madarakani) anaweza kushtakiwa binafsi kufuatia matendo yake au kukiuka Katiba.

Katiba inasema mashtaka ambayo hawezi kufunguliwa ni ya uhalifu, wakati akiwa mamlakani.

You can share this post!

Aguero kuyoyomea Barcelona mwishoni mwa msimu

DOUGLAS MUTUA: Suluhu itafutwe kwa vita kati ya Israeli na...