Habari MsetoSiasa

BBI: Mashirika ya kamari ya kibinafsi kuharamishwa

November 28th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

KAMPUNI za kamari za kibinafsi huenda zikapigwa marufuku nchini endapo ripoti ya BBI itatekelezwa na serikali.

Badala yake, ripoti hiyo inapendekeza kubuniwa kwa kampuni moja itakayomilikiwa na serikali kuendesha biashara ya kamari.

“Kampuni za kamari za kibinafsi zinazidi kuwafanya vijana kuwa maskini hohehae. Jopo hili linapendekeza kubuniwa kwa kampuni ya serikali ambalo mapato yake yatatumiwa katika kuboresha maisha ya vijana, michezo, utamaduni na shughuli nyinginezo za kijamii,” inasema ripoti. Kampuni za kamari Sportpesa na Betin tayari zimesimamisha operesheni zao nchini kwa madai kuwa zilihangaishwa na serikali.

Sportpesa na Betin zilikuwa miongoni mwa kampuni 19 za kamari zilizopokonywa leseni kwa kukwepa kulipa ushuru.

Jopo hilo linataka serikali kubuni sheria kali ya kudhibiti mikopo inayotolewa kwa njia ya simu kutokana na kile linachosema ‘inawaletea’ umaskini Wakenya.

“Kuna haja ya kubuni sheria kali ya kudhibiti mikopo ya simu ambayo inaumiza Wakenya maskini kwa kuwatoza riba ya juu,” inasema..

Jopokazi la BBI pia limeonya serikali dhidi ya kuchukua mikopo kutoka katika mataifa ya kigeni.

“Usiwatwike watoto wetu mzigo mzito wa madeni kwani watateseka katika siku za usoni. Kizazi cha sasa hakifai kuumiza kizazi kijacho,” inaonya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo pia inapendekeza kuwa vijana wapate ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kufanya biashara katika Vituo vya Huduma.Ushauri huo utatolewa na wataalamu ambao wamebobea katika masuala ya biashara. Waziri wa Huduma za Umma, Vijana na Jinsia Margaret Kobia, miezi miwili iliyopita, alisema idadi kubwa ya vijana hawana maarifa ya kuendesha biashara.

Kulingana na Bi Kobia, ni asilimia 20 tu ya vijana ambao wakipata hela za mradi wanaweza kufungua biashara.

Jopo hilo pia linapendekeza vijana wanaoanzisha biashara wasitozwe ushuru kwa kipindi cha miaka saba.

“Wakenya wanafaa kuanza kupewa ujuzi wa kuendesha biashara katika umri mdogo,” inasema ripoti.

“Serikali inafaa kubuni mbinu za kufadhili vijana wenye vipaji vya muziki, michezo uigizaji, nakadhalika. Hatua hiyo itatoa hamasa kwa vijana kujiboresha zaidi,” inasema ripoti hiyo.