Habari MsetoSiasa

BBI: Maspika sasa kuteua manaibu gavana

November 27th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Magavana wanaokosa kuteua manaibu wao katika muda wa siku 90 nafasi ikitokea, watakapokonywa jukumu hilo na maspika wa mabunge ya kaunti zao, ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) inapendekeza.

Ripoti hiyo inasema kwamba, gavana akikosa kuteua naibu wake katika muda wa miezi mitatu akijiuzulu au kufa, spika wa bunge la kaunti, kwa idhini ya bunge lake, atateua naibu gavana.

Hii inanuiwa kukabiliana na hali kama iliopo katika kaunti ya Nairobi ambapo Gavana Mike Sonko amekataa kuteua gavana kwa takriban miaka miwili sasa.

Ikitekelezwa, gavana na naibu wake hawatakuwa wa jinsia moja kwa sababu kila mgombeaji atakuwa akiteua mgombea mwenza wa jinsia tofauti.

Ripoti hiyo inapendekeza kuwa ugatuzi uimarishwe kwa kudumisha kaunti zote 47, kisha zitengewe pesa zaidi, na serikali igatue majukumu yote ya serikali za kaunti inayokwamilia.

Kulingana na ripoti hiyo, ugatuzi umefaulu mno nchini na changamoto zilizopo zinaweza kutatuliwa.

“Kaunti zote 47 zidumishwe lakini zihimizwe kuunda miungano ya kimaeneo ya kiuchumi kwa hiari,” inasema ripoti iliyokabidhiwa Rais Kenyatta.

Wakenya walifahamisha kamati iliyokusanya maoni kuwa wangetaka serikali za kaunti zitengewe asilimia 35 ya mapato ya serikali kwa kutegemea pesa zilizokusanywa mwaka uliotangulia.

Kwa sasa, katiba inasema zinapaswa kutengewa angalau asilimia 15 ya mapato ya kitaifa.

Ripoti inaeleza kuwa Wakenya wanataka mfumo utakaohakikisha kuwa pesa zitafikia Wakenya mashinani ili pesa sizitengwe kwa kutegemea ukubwa wa eneo.

Hii inamaanisha kuwa maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu yanapaswa kutengewa pesa nyingi kuliko yaliyo na watu wachache.

Kulingana na ripoti hiyo, Wakenya wanahisi kwamba hatua ya serikali ya kitaifa ya kukwamilia baadhi ya majukumu ambayo kikatiba yanafaa kuwa yamegatuliwa, kumenyima serikali za kaunti pesa za kufanikisha maendeleo kwa kuwa kila jukumu linapaswa kutengewa pesa za kulifanikisha.

Ili kuhakikisha pesa zimefika mashinani, ripoti inapendekeza mikakati ya kuhakikisha miradi imefadhiliwa katika kila wadi na kwa njia ya uwazi na uwajibikaji katika kila kipindi cha miaka mitano.

Ili kukomesha migomo ya wahudumu wa afya ambayo imekuwa ikilemaza huduma katika kaunti, ripoti inapendekeza kubuniwe tume huru ya huduma ya afya.

Tume hii itahakikisha kuwa hakuna eneo litakalokosa wataalamu katika sekta hiyo ambao ni wachache.Ili kukabiliana na matumizi mabaya ya pesa katika serikali za kaunti ukiwemo ufisadi, ripoti inapendekeza zipigwe darubini na mashirika yanayoweza kuwajibika ili kuhakikisha pesa nyingi zinatengewa miradi ya maendeleo.

Ripoti inasema sheria ipitishwe ili asilimia 70 ya pesa za kaunti zinapaswa kutumiwa kwa miradi ya maendeleo huku asilimia 30 ikitumiwa kuendesha serikali.

Kulingana na ripoti hiyo, magavana watakuwa wakikamilisha miradi iliyoanzishwa na watangulizi wao kwanza kwa kunyimwa pesa za miradi mipya.

Ikiwa gavana anataka kuacha mradi ulionzishwa na mtangulizi wake, atalazimika kupatia umma sababu ya kuridhisha, inaeleza ripoti hiyo.

Mapendekezo mengine ni kukomesha marupurupu ya vikao ya watumishi wa umma wanaolipwa mishahara wanayopata wakifanya mikutano.