Habari MsetoSiasa

BBI: Mimi na Raila pia tulikuwa na hofu – Uhuru

November 28th, 2019 1 min read

Na JUMA NAMLOLA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alisimulia jinsi yeye na kinara wa ODM Raila Odinga walivyonyamaziana kwa karibu saa nzima kabla ya kuanza mazungumzo yaliyozaa handisheki.

Mazungumzo hayo ndiyo chimbuko la ripoti iliyokusanywa na Jopo la Maridhiano (BBI).

Akizungumza katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi, Rais Kenyatta alieleza jinsi yeye na Bw Odinga walivyojifungia kwenye chumba wakiwa hawasemi chochote isipokuwa kunywa chai na kujuliana hali.

Alisema sababu kubwa iliyosababisha taharuki na chuki miongoni mwao ni kuwa kila mmoja alikuwa anahisi kuwa ndiye aliyestahili mamlaka makuu ya kuongoza nchi.

Bw Odinga alikuwa ametoka kuapishwa kuwa ‘Rais wa wananchi’ katika uwanja wa Uhuru Park mnamo Januari 30, 2018 baada ya kushawishi wafuasi wake kususia marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, 2017.

“Hiyo hofu mliyokuwa nayo, hata sisi tulikuwa nayo pia. Huyu mtu tukikutana naye, tutaambiana nini? Tutasema nini? Na kwa kweli wakati tulipokutana, tulikunywa chai kwa dakika 45 hakuna mazungumzo ila tu kuulizana mambo ya familia.”

“Hakuna maneno yanaweza kutoka kwa sababu ya hasira ya yale tulikuwa tumerushiana hapo mbele. Baada ya saa moja hivi ndipo mambo yakaanza. Na tukasema kitu kimoja baada ya kumaliza mazungumzo: Tofauti zetu sio kubwa vile. Mashindano, ndiyo yanayotuletea shida hizi zote…,” akasema Rais.