Habari MsetoSiasa

BBI: Mivutano ya kisiasa yatarajiwa

November 28th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

SAFARI ya kujadili na hatimaye kutekeleza ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), ambayo ilitolewa rasmi kwa umma jana katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi, itakuwa ndefu na yenye panda shuka nyingi.

Hii ni kwa sababu ya mchakato wa kisheria unaohusika na vitisho vya baadhi ya wabunge kuipinga.

Rais Uhuru Kenyatta ameahidi kwamba atatekeleza ripoti hiyo kikamilifu ingawa baadhi ya wanasiasa wa chama chake cha Jubilee wametishia kuipinga.

Mshirika wa Rais Kenyatta katika handisheki iliyozaa jopokazi lililoandaa ripoti hiyo, Raila Odinga, amekuwa akiipigia debe ripoti hiyo na kuwataka wanaoipinga kuisoma kwanza.

Kulingana na Rais Kenyatta na Bw Odinga, ripoti hiyo itakuwa mwanzo wa kuunganisha Wakenya ambao wamekuwa wakipingana wakati wa uchaguzi kila baada ya miaka mitano baadhi ya jamii zikihisi kutowakilishwa katika serikali

Jana, ilikuwa dhahiri mjadala utakuwa mkali wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen na mwenzake katika bunge la taifa Aden Duale walipotofautiana na wanenaji wengine katika uzinduzi wa ripoti hiyo.

Dkt Ruto mwenyewe alisisitiza kuwa mjadala kuhusu ripoti hiyo haufai kutumiwa kubuni nafasi za kazi kwa watu wachache.

Ripoti hiyo sio mswada mbali ni mapendekezo kutoka kwa maoni ambayo jopokazi hilo lilikusanya kutoka kwa Wakenya wapatao 7,000.

Rais Kenyatta amekuwa akisisitiza kuwa baada ya kuipokea, itawasilishwa kwa Wakenya ili waijadili na kutoa mchango wao, shughuli iliyoanza jana kwenye kikao cha Bomas.

“Tutarudi na BBI hivi karibuni na yeyote asiwadanganye kuwa ni siasa tutakuwa tukifanya,” Rais Kenyatta alisema alipokuwa akizindua ripoti hiyo.

Alichomaanisha ni kuwa yeye na Bw Odinga watazunguka nchini kukutana na wananchi kupigia debe ripoti hiyo.

Kama ingependekeza mabadiliko ya kisheria yanayohusu kipindi cha rais na ugatuzi miongoni mwa masuala mengine mswada hungeundwa kuwasilishwa kwa mabunge yote 47 ya kaunti nchini ujadiliwe.

Mswada huo ungehitajika kupitishwa na mabunge ya kaunti 24 kabla ya kuwasilishwa kwa bunge la taifa.

Iwapo kwenye mjadala kuhusu ripoti hii Wakenya hawatapendekeza kura ya maamuzi kufanyika, mswada utaandaliwa na kuwasilishwa ujadiliwe katika bunge la taifa ambako mdahalo mkali unatarajiwa.