Habari

BBI: Mlima Kenya wapigia Uhuru debe 'Tangatanga' wakizomewa

March 1st, 2020 2 min read

BENSON MATHEKA NA MARY WANGARI

VIONGOZI wa eneo la Mlima Kenya, Jumamosi walitumia mkutano wa hamasisho la Mpango wa Maridhiano (BBI) mjini Meru kumpigia debe Rais Uhuru Kenyatta kubaki uongozini baada ya kukamilisha kipindi chake cha pili mwaka wa 2022.

Waliozungumza kwenye mkutano huo walisema kwamba Uhuru ataendelea kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya hata baada ya 2022.

Gavana wa Nyandarua, Bw Francis Kimemia alisema hakuna pengo la msemaji katika eneo la Mlima Kenya.

“Hatuna pengo la uongozi. Kiongozi wetu Mlima Kenya ni Uhuru Kenyatta na kwa hilo hatuombi yeyote msamaha. Wale wanaosema kuna pengo wajue hivyo,” alisema.

Walisisitiza kuwa hakuna kitakachomzuia Rais Uhuru kugombea wadhifa wowote wa kisiasa baada ya katiba kufanyiwa mageuzi kupitia BBI.

Viongozi waliozungumza katika mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Kinoru, walisema kwamba hawatambui msemaji mwingine wa kisiasa eneo lao.

Akihutubia maelfu ya wakazi waliohudhuria hafla hiyo, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, Bw David Murathe alisema Rais Uhuru hataachia mamlaka mtu asiyeweza kuaminika.

“Hatutauziwa uoga, Uhuru hataachia mwizi kiti. Mnataka Rais amwachie mwizi mamlaka? Hilo halitatendeka,” alisema Bw Murathe.

Magavana, wabunge na viongozi wa vyama vya kisiasa walisema kwamba BBI itabadilisdha siasa nchini.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli alisema kuwa baada ya katiba kubadilishwa, Rais Uhuru atapata kiti cha uwaziri mkuu akimaliza enzi yake kama rais. Katika hatua ambayo haikutarajiwa, wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Tangatanga wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet walipewa fursa ya kuzungumza katika mkutano huo.

Bw Murkomen alizomewa na umati alipowakashifu wanasiasa aliodai wanawapotosha Wakenya kupitia BBI.

“Lazima tuanze na ukweli ndipo taifa letu liweze kusonga mbele. Shida kubwa ya siasa Kenya ni utapeli, tukitaka kuunganisha Wakenya tuache utapeli kila mmoja apate nafasi ya kusema anachotaka kusema,” alieleza Bw Murkomen.

Kiongozi huyo wa Wengi ambaye ni mwandani wa karibu wa Naibu Rais, pia aliwahimiza wanasiasa kumheshimu Naibu Rais sawa na jinsi wanavyotaka Rais Uhuru aheshimiwe.

“Tuache uongo kwa raia kwamba tusubiri BBI ili tusuluhishe matatizo ya Wakenya. Tulichaguliwa 2017 kusuluhisha shida za Wakenya na tumepewa pesa tulete maendeleo kwa Wakenya. Tubadilishe Kenya kulingana na mkataba tuliokubaliana nao,” alisema.

Kisanga kilizuka katika hafla hiyo wakati Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria aliondoka kwa hasira baada ya Murkomen kuzomwa.