Habari Mseto

BBI: Mtihani kwa Matiang'i 'Reggae' ikianza

November 1st, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

KUZINDULIWA kwa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) Jumatatu na Rais Uhuru Kenyatta kunatarajiwa kuongeza kibarua cha Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i katika kudhibiti mazingira ya kisiasa nchini.

Dkt Matiang’i ndiye Mratibu Mkuu wa Kamati ya Kitaifa Inayosimamia Miradi ya Serikali (NGPCC), ambayo inajumuisha mawaziri wote ambao wizara zao zimetwikwa jukumu la kuendesha miradi muhimu ya kitaifa.

Kwa mujibu wa wadadisi, macho yote yatakuwa kwake kuhusu vile atadhibiti mazingira ya kisiasa nchini, kwani kando na kampeni za kuipigia debe BBI, siasa za uchaguzi mkuu 2022 zitakuwa zimeanza kuchacha.

Kundi la Tangatanga limekuwa likimlaumu waziri na Katibu wa Wizara, Dkt Karanja Kibicho kuwa ‘vibaraka’ wa serikali kwa kuwatumia polisi kusambaratisha baadhi ya mikutano yao.

Kwenye ziara yake katika Kaunti ya Kisii wiki iliyopita, Rais Kenyatta alimtetea vikali Dkt Matiang’i, akiirai jamii ya Abagusii kujitokeza wazi ‘kumtetea mtoto wao’ dhidi ya wakosoaji wake.

“Lazima mumtetee mtoto wenu dhidi ya wale wanaomtukana anapotekeleza kazi yake. Sharti muwe tayari kumlinda,” akasema Rais Kenyatta.

Ingawa kauli hiyo ilionekana kumlenga Naibu Rais William Ruto na kundi la Tangatanga, wadadisi wanasema ilionyesha imani kubwa aliyo nayo Rais Kenyatta kwa Dkt Matiang’i, na inaashiria ‘umuhimu wake kwa Rais hasa wakati huu yuko kwenye mkondo wa lala salama kwa muhula wake.’

Kumekuwa na vumi kuwa huenda waziri huyo anaandaliwa kwa wadhifa mkubwa zaidi wa kisiasa baada ya 2022, wadadisi wakiamini mtihani mkuu kwake utakuwa jinsi atakavyosimamia siasa za BBI.

“Dkt Matiang’i ameibukia kuwa mshirika wa karibu zaidi wa Rais Kenyatta na anayemwamini kusimamia masuala muhimu yanayohusu miradi ya Serikali. Ingawa amewakasirisha wandani wa Dkt Ruto kwa kuonekana kuchukua baadhi ya majukumu yake, ameendelea kudumisha imani ya kuwa mchapakazi anayeaminika,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kabla ya kuteuliwa kwenye baraza la mawaziri 2013, Dkt Matiang’i alihudumu kama mhadhiri wa Fasihi ya Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Nairobi.