Habari MsetoSiasa

BBI: Muturi azima ndoto ya Tangatanga

December 2nd, 2019 2 min read

JUSTUS OCHIENG Na LEONARD ONYANGO

WANASIASA wa kundi la Tangatanga wamepata pigo baada ya Spika Justin Muturi kusema kuwa hatakubali ripoti ya BBI kuwasilishwa bungeni.

Bw Muturi aliyekuwa akizungumza wakati wa mkutano wa kuchangisha fedha kanisani katika eneobunge la Uriri, Kaunti ya Migori, alisema ripoti ya BBI ni ya wananchi na ni sharti iwasilishwe kwa Wakenya wafanye uamuzi wa mwisho.

Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanataka kuandaliwa kwa kura ya maamuzi ili Wakenya wapitishe yaliyomo katika ripoti ya BBI.

Kwa upande mwingine, Naibu wa Rais William Ruto pamoja na wanasiasa wanaomuunga mkono wa kundi la Tangatanga wanataka ripoti ya BBI itekelezwe kupitia bungeni.

Dkt Ruto anashikilia kwamba hakuna haja ya kuandaa kura ya maamuzi kwani mapendekezo yaliyo kwenye ripoti ya BBI yanaweza kutekelezwa kupitia bungeni.

Akizungumza jana katika eneo la Kimende, Kaunti ya Kiambu alipoongoza hafla ya kufuzu kwa watu waliokuwa wakisoma kozi fupi kupitia ufadhili wa Hazina ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF), Dkt Ruto aliwataka wanaotaka ripoti ya BBI kupelekwa kwa wananchi kukoma kutishia wanaotaka ipelekwe bungeni.

“Wanaotaka kufanyika kwa kura ya maamuzi wakome kutishia wanaopinga kwa sababu maoni ya kila mtu yanafaa kuheshimiwa. Tutekeleze mapendekezo ya ripoti ya BBI bila kugawanya Wakenya,” akasema Dkt Ruto.

Wabunge wa Tangatanga tayari wameanzisha njama ya kutaka kuandaa mswada utakaojumuisha mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti ya BBI na kuuwasilisha bungeni.

Lakini Bw Muturi jana alisema hataruhusu mswada huo kuwasilishwa bungeni.

“Ripoti ambayo imetoka kwa wazee ni ya Wakenya na haiwezi kuletwa bungeni. Mswada kuletwa bungeni ni lazima niidhinishe,” akasema Bw Muturi katika hafla iliyohudhuriwa na mbunge wa Uriri Mark Nyamita na Seneta wa Migori Ochillo Ayacko.

Viongozi wengine waliokuwepo ni mwenyekiti wa ODM John Mbadi, Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni na wabunge Tim Wanyonyi (Westlands) na Maisora Kitayama (Kuria Mashariki).

“Mambo ambayo yako ndani ya ripoti ya BBI ni yetu sisi sote kama Wakenya. Tuwaunge mkono viongozi wetu ili tulete amani na uwiano nchini,” akasema Bw Muturi.