HabariSiasa

BBI ni daraja la Canaan – Raila

January 11th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA NA RUTH MBULA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amesema mchakato ulioanza Ijumaa wa kuvumisha mapendekezo kwenye ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) unalenga kuwafikisha Wakenya Canaan (yaani kuboresha maisha yao).

Akihutubia zaidi ya wajumbe 3,000 waliohudhuria mkutano wa kwanza wa aina hiyo jana mjini Kisii, Bw Odinga alisema BBI inalenga kufikia lengo hilo kwa kuunganisha Wakenya kote nchini.

“Tumeanza safari ya Kenya moja, watu wamoja hapa Nyanza. Tunaelekea Canaan kwa kujenga madaraja ya kuunganisha wananchi kutoka pembe zote za nchi,” Bw Odinga akasema katika uwanja wa michezo wa Kisii Sport Club.

Mkutano huo ulihudhuriwa na mawaziri Fred Matiang’I (Usalama wa Ndani), Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na zaidi ya Magavana 20, kando na sita kutoka eneo la Nyanza wakiongozwa na mwenyeji Gavana wa Kisii James Ongwae. Pia walikuwepo maseneta na wabunge kadhaa kutoka kaunti zote sita za Nyanza.

Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa Chama cha ODM alifichua kuwa, ipo mipango ya kuandiliwa kwa mikutano aina hiyo ya Kisii katika maeneo yote nchini ikiwemo eneo la Mlima Kenya ambako wanasiasa wengine wamekaidi Rais Uhuru Kenyatta.

“Tumeanza safari na tutazuru sehemu zote kuwahamasisha Wakenya kuhusu BBI. Baada ya hapa Kisii, tutaelekea uwanja wa Bukhungu, Kakamega juma lijalo (Januari 18). Kisha tutaenda Mombasa, Embu, Eldoret, Garissa, na hata kaunti za eneo la Kati mwa Kenya,” Bw Odinga akasema.

Mkutano ujao mjini Kakamega tayari umegawanya viongozi wa magharibi mwa Kenya huku kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula na baadhi ya wabunge wa huku wakiupinga wakidai unalenga kuwahujumu kisiasa.

Bw Odinga, alikariri kujitolea kwake kushirikiana na Rais Kenyatta kwa ajili ya kuwaunganisha Wakenya na kuziba mianya ya migawanyiko miongoni mwa Wakenya inayosababishwa na tofauti zinazoibuliwa na matokeo ya chaguzi kila baada ya miaka mitano.

Uwepo wa mawaziri Matiang’i na Wamalwa ulikuwa ishara tosha kwamba mkutano huo uliidhinishwa na Kiongozi wa Taifa.

Baadhi ya magavana wengi waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na mwenyekiti wa baraza la magavana nchini ambaye pia ndiye gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, Anne Waiguru (Kirinyaga), Kivutha Kibwana (Makueni), Hassan Joho (Mombasa), Cypria Awiti (Homa Bay), Okoth Obado (Migori), John Nyagarama (Nyamira) , Anyang’ Nyong’o (Nyamira), Cornel Rasanga (Siaya) miongoni mwa wengine.

Kabla ya mkutano huo kuanza, Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi alidai maisha yake yamo hatarini kwa kuupinga.

Akiongea na wanahabari mjini Kisii, Bw Maangi ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto alidai jana alfajiri watu alioamini kuwa maafisa wa polisi walivamia boma lake na kutwaa magari yake rasmi.

“Mwendo wa saa kumi alfajiri leo (jana) takriban maafisa 12 walifika nyumbani kwangu mjini wakiwa na mitambo ya kuburuta magari niliyopewa na serikali ya kaunti lakini wafanyakazi wangu wakawapa vifunguu na watatwaa magari hayo,” akawaambia wanahabari mjini Kisii.

“Sasa nahisi kuwa maisha yangu yamo hatarini kwa sababu mnamo Jumatatu usiku, gari lenye nambari ya usajili ya serikali ilinifuata nikisafiri kutoka Nairobi kwenda Kisii. Lakini nililikwepa kwa kubadili barabara,” Bw Maangi akaongeza.

Na kwenye ujumbe aliyoandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook Naibu huyo wa Gavana alikariri kuwa, kuna watu fulani wanaotaka kumwangamiza ili kuzima ndoto yake ya kuwania ugavana wa Kisii 2022.