Siasa

BBI ni daraja la kutufikisha Canaan – Uhuru

November 12th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya kuunga mkono mswada kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) huku akisema utawafikisha ‘Kanani’.

Akihutubia Bunge Alhamisi, Rais aliorodhesha mambo mema ambayo Wakenya watapata baada ya kubadilisha Katiba na kujumuisha mapendekezo yaliyomo katika ripoti ya BBI.

“Sawa na Musa katika Biblia aliyeketi juu la Mlima Nebo na kuona siku za mbele Waisraeli walipokaribia kuvuka na kuingia katika Nchi ya Ahadi (Kanani), mimi pia nimeona siku za mbele,” akasema Rais Kenyatta.

“Huko mbele hakutakuwa na mtu ambaye atashikilia afisi ya juu kwa sababu ya makabila yao. Hakuna mtu atazama kwenye umaskini kutokana na utawala mbaya. Nimeona Kenya ambapo watu waliohitimu hawataumizwa na umaskini,” akaongezea.

Kiongozi wa nchi alisema kuwa, rasilimali za nchi zitagawanywa kwa usawa kote nchini baada ya kupitishwa kwa BBI na maisha yatakuwa raha mustarehe.

Rais Kenyatta aliwataka Wakenya kusoma kwa makini mswada wa BBI ili wafanye uamuzi ufaao.

“Tujadiliane kwa ustaarabu ili tuweze kutatua changamoto zinazokumba taifa letu. Tuangamize ukabila na tupambane na ufisadi,” akasema. Rais, hata hivyo, hakusema ikiwa mswada huo wa BBI utafanyiwa marekebisho ili kujumuisha mapendekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na makundi mbalimbali; yakiwemo magavana, madiwani, viongozi kutoka maeneo ya wafugaji na viongozi wa dini.

Magavana wanataka watengewe fedha za kiinua mgongo ili waishi raha mustarehe baada ya kustaafu.

Magavana pia wanapendekeza waruhusiwe kuteua manaibu wao baada ya kuchaguliwa tofauti na sasa ambapo wanachaguliwa pamoja.

Mswada wa BBI unapendekeza kuwa gavana na naibu wake wawe watu wa jinsia tofauti; lakini magavana wamepinga vikali pendekezo hilo.

Nao madiwani wanataka wapewe magari ya bwerere ya kati ya Sh2 milioni na Sh4 milioni. Madiwani, vilevile, wanataka Kifungu cha 22 (1)(b) (ii) cha Sheria za Uchaguzi 2016 kinachotaka madiwani na wabunge kuhitimu kiwango cha digrii kifutiliwe mbali.

“Hitaji la kutaka madiwani kuwa na shahada ya digrii litafanya nyadhifa za kisiasa kuwa za wasomi na kutenga viongozi wengine ambao hawakupata fursa ya kuendeleza masomo yao katika vyuo vikuu,” akasema Ndegwa Wahome kiongozi wa jukwaa la madiwani. Kiongozi wa ODM Raila Odinga, amesema hakuna mambo mapya yataingizwa ndani ya mswada huo.