Habari Mseto

BBI ni ya wakora wa kisiasa, haifai raia, adai Aukot

November 30th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE na PIUS MAUNDU

KIONGOZI wa Chama cha Third Way Alliance Ekuru Aukot amepuuzilia mbali mapendekezo katika ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) akisema yanalenga kuwafaidi wanasiasa wala sio mwananchi wa kawaida.

Hata hivyo, magavana ambao walikuwa wakishinikiza kura ya maamuzi ya Ugatuzi Initiative walisema wataiunga mkono.

Dkt Aukot ametangaza kuwa ameunda upya mswada wake wa Punguza Mizigo, uliokataliwa na mabunge ya kaunti na kwamba atauzindua upya wiki ijayo.

“Ripoti hii ya BBI haina mapendekezo yenye manufaa kwa mwananchi wa kawaida. Ripoti hii inaendeleza maslahi ya wanasiasa, jambo ambalo lilidhihirika wazi katika hafla ya uzinduzi wake katika ukumbi wa Bomas of Kenya,” akasema.

“Ripoti hii imewagawanya Wakenya zaidi kuliko vile walivyokuwa kabla ya handisheki kwani imechochea mashindano ya kisiasa,” Dkt Aukot akaongeza kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Alikosoa pendekezo la kurejeshwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu akisema hautawasaidia Wakenya bali wanasiasa wachache “wenye kiu ya uongozi”.

“Wanachama 14 wa jopokazi hilo hawakuwa na imani kwa ripoti yenyewe na ndiyo maana walikodi watalaamu kuwachambulia wananchi mapendekezo yake. Hii ina maana kuwa yaliyomo kwenye ripoti hiyo hayaakisi maoni na mapendekezo ya wananchi bali ya watu ambao walilipa jopokazi hilo kazi hiyo,” akasema Bw Aukot.

Vilevile, kiongozi huyo wa chama cha Thirdway Alliance aliwasuta wanachama wa jopo la BBI kwa kuhujumu uhuru wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kupendekeza kuwa vyama vya kisiasa viwe na usemi katika uteuzi wa makamishna wa tume hiyo.

“Hii ni sawa na kuwapa washindani katika mchezo huu wa kisiasa nafasi ya kuteua refarii. Hatua kama hii itayeyusha mamlaka ya tume hii inayopaswa kuwa huru,” Dkt Aukot akasema.

Alisema mswada mpya wa Punguza Mizigo sasa utakuwa na mapendekezo ambayo yatakubalika na mabunge yote ya kaunti.

“Mswada wetu sasa umefanyiwa marekebisho na unajumuisha masuala yote ambayo hayakuwa katika rasimu ya kwanza,” akasema Dkt Aukot.

Akaongeza: “Mswada huu mpya unalenga matakwa ya wananchi. Umenakili mikakati ya kupambana na ufisadi, kuimarisha ugatuzi na kupunguza kero la uwakilishi kupita kiasi.”

Mswada wa Punguza Mizigo ulikataliwa na takribani mabunge 31 mnamo Agosti 2019 yakisema mapendekezo yake hayangeweza kutekelezwa kwa urahisi. Ni Kaunti za Uasin Gishu na Turkana pekee zilizoupitisha.

Wakati huo huo magavana wanapanga kusitisha mpango wao wa kushinikiza mageuzi ya Katiba kufuatia kuzinduliwa kwa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI). Gavana Kivutha Kibwana wa Makueni alisifu mapendekezo yaliyotolewa na ripoti ya jopo hilo ambayo ilizinduliwa Jumatano na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Profesa Kibwana ni mwenyekiti mwenza wa mpango wa Ugatuzi Initiative unaoendeshwa na magavana kushinikiza kuandaliwa kwa kura ya maamuzi. Alisema masuala mengi ambayo magavana walikuwa wakipendekeza yamejumuishwa katika ripoti hiyo.

“Kamati ya Katiba katika Baraza la Magavana (CoG) itaketi na kutathmini ripoti ya BBI ili tuweze kuwashauri magavana kuhusu mwelekeo tutakaochukua. Tutaunganisha mjadala wa mchakato wetu na ule wa BBI kwa kuwa ripoti hiyo inapendekeza mambo mengi ambayo tulikuwa tumependekeza.